HABARI MPENZI MWANAMICHEZO KARIBU KATIKA KURASA HII MAHSUSI KWA HABARI ZA MICHEZO PIA UNAWEZA KUTANGAZA BIASHARA YAKO HAPA KWA BEI NAFUU ZAIDI KWA MUDA MREFU ZAIDI WASILIANA NASI KWA NAMBA +255713 15 33 48

13 May 2013

HARUNA NIYONZIMA AMUWAZA MAFISANGO KUMKUMBUKA JUMAMOSI


 

 Kiungo tegemeo wa mabingwa wapya wa Ligi Kuu ya Tanzania Bara msimu huu 2012/ 2013 Yanga, Haruna Niyonzima, amesema kuwa ana furaha ya kuona timu yake imefanikiwa kutwaa ubingwa wa ligi hiyo lakini amekuwa hana raha akiiwaza mechi dhidi ya watani wa jadi, Simba ambayo inamkumbusha 'ndugu' yake, marehemu Patrick Mafisango.

Mafisango alifariki dunia Mei 16 mwaka jana kwa ajali ya gari na mwaka huu Mei 18 siku watani hao wanapokutana katika mchezo wa funga dimba atakuwa tayari ameshatimiza mwaka mmoja tangu alipoaga dunia.

Niyonzima alikuwa ni mmoja wa watu waliosafiri kuelekea Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo kwenda kuhudhuria mazishi ya kiungo huyo ambaye asili yake ni nchi hiyo.

  Niyonzima, amesema kwamba mechi hiyo kwake anaiona ngumu kutokana na kila mara kukumbuka maneno ya mwisho ambayo marehemu Mafisango alimueleza wakati wanabadilishana jezi baada ya mchezo ambao Yanga ililala 5-0 ulipomalizika.

Niyonzima alisema kwamba anaumia sana kila anapomkumbuka marehemu Mafisango ambaye alicheza naye kwenye timu inayoshiriki Ligi Kuu ya Rwanda, APR na timu ya Taifa ya nchi hiyo (Amavubi) kabla ya wote kuja Tanzania Bara kucheza soka la kulipwa.

"Kila tulipokuwa tunakaribiana uwanjani alikuwa akiniambia kwa Kinyarwanda kwamba nifanye kazi yangu iliyonileta Tanzania, nisisikilize maneno ya watu na aliniambia nitabadilishana na yeye (Mafisango) jezi baada ya mechi kuisha na hadi sasa ninayo nyumbani nimeitunza," alisema Niyonzima.

Alisema anaamini kwake deni kwa Yanga msimu huu lilikuwa ni kuipa mafanikio ya kutwaa ubingwa na kuhakikisha wanalipiza kisasi cha kuwafunga watani zao ili kukamilisha sherehe za kunyakuwa kikombe hicho cha ligi ya juu Tanzania Bara.

Niyo anasema kwamba msimu huu wa pili akiichezea Yanga umekuwa na mafanikio kwa sababu alianza kwa kutwaa ubingwa wa mashindano ya Klabu Bingwa Afrika Mashariki na Kati (Kombe la Kagame) na kumaliza na kutwaa ubingwa wa ligi hivyo anaamini ameisaidia Yanga kupata mafanikio kama walivyotarajia wakati wanamsajili.

MSIMU UJAO
Kiungo huyo ambaye Desemba mwaka jana alitakiwa na klabu ya El Mereikh ya Sudan aliweka wazi kwamba bado hajajua hatma yake kutokana na kutosaini mkataba na timu yoyoye hadi jana mchana.

Niyonzima alisema kuwa hatakurupuka kufanya maamuzi kwa sababu anajua soka ndiyo linaloendesha maisha yake ya kila siku pamoja na familia.

"Sitakurupuka, nimeshazungumza na watu mbalimbali ndani na nje ya nchi lakini sijafanya maamuzi ya mwisho," alimaliza nyota huyo anayevaa jezi namba 8 akiwa na Amavubi, APR na sasa Yanga.

Aliwataka mashabiki na wapenzi wa Yanga wasiwe na wasiwasi kwa sababu kwa sasa akili yake ipo kwa ajili ya kuitumikia klabu hiyo hadi mwisho wa msimu

No comments:

Post a Comment

lisungu_chisara@yahoo.com

TUTUMIE HABARI YOYOTE YA MICHEZO, BURUDANI TUTAZICHAPISHA

TANGAZA KWA MFUMO HUU


MAHUDHURIO YA WASOMAJI KIMATAIFA

free counters

Followers