HABARI MPENZI MWANAMICHEZO KARIBU KATIKA KURASA HII MAHSUSI KWA HABARI ZA MICHEZO PIA UNAWEZA KUTANGAZA BIASHARA YAKO HAPA KWA BEI NAFUU ZAIDI KWA MUDA MREFU ZAIDI WASILIANA NASI KWA NAMBA +255713 15 33 48

15 May 2013

KMKM JIANDAENI KABISA MSISUBILI KUTULETEA VISNGIZIO

HATIMAE ligi kuu ya soka Zanzibar imefikia tamati huku timu ya Kikosi Maalum cha Kuzuia Magendo, KMKM ikitawazwa rasmi ubingwa wa historia.
Hatua hiyo imeifanya timu ya wanamaji hao kupata tiketi ya kuiwakilisha Zanzibar katika michuano ya ligi ya mabingwa barani Afrika, na ile ya Kombe la Kagame kwa nchi za Afrika Mashariki na Kati hapo mwakani.

Aidha, kukamilika kwa ligi hiyo, kunatoa nafasi kwa timu ya Chuoni iliyoshika nafasi ya pili miongoni mwa timu 12 zilizokuwa zikitoana jasho katika ngarambe hizo msimu uliomalizika, kupeperusha bendera ya Zanzibar kwenye mashindano ya kuwania Kombe la Shirikisho Afrika (CAF).

Awali ya yote, sina budi kuzipongeza timu mbili hizo kwa mafanikio waliyopata, kwani hakika yametokana na kazi ngumu, bidii na kujituma, pamoja na kujiandaa vizuri.
Aidha, nitakuwa mwizi wa fadhila kama sitakipongeza Chama cha Soka Zanzibar (ZFA) Taifa, kwa umakini wapo katika kusimamia ligi ya mwaka huu, licha ya kasoro mbalimbali zilizojitokeza.
Ni jambo la kufurahisha kwamba ligi ya msimu huu imemalizika kwa wakati bila kalenda yake kupitwa na muda, ingawa tamati yake haikushirikisha timu zote 12 siku ya mwisho ya kufunga pazia la ligi hiyo.
Kwa mara ya kwanza, tumeshuhudia ligi yetu ikiendana na kalenda ya kimataifa, ingawa huko Ulaya na kwengineko, ligi zimebakisha kati ya mzunguko mmoja na miwili, ambayo si tafauti kubwa na hii ya kwetu iliyomalizika tarehe 4 mwezi huu.
KMKM imekuwa bingwa wa kihistoria kutokana na ligi kuu msimu huu kupata baraka kubwa ya kudhaminiwa na kinywaji cha Grand Malt, hivyo kuwa timu ya kwanza kuchukua ubingwa chini ya udhamini huo.
Kwa hatua hiyo, mabingwa hao walikabidhiwa kitita cha shilingi milioni kumi zikiwa zawadi kwa ushindi huo, na Chuoni ikipata shilingi milioni tano, kama ilivyoahidiwa na wadhamini hao.
Tunaishukuru Grand Malt kwa kukisikia na kukinyamaza kilio cha miaka mingi cha Wazanzibari kilichotokana na kukosa udhamini wa ligi hiyo, na hivyo kuanza kurejesha matumaini yaliyokuwa yameanza kutoweka, kwa soka la Zanzibar kukosa mvuto.
Sasa baada ya yote hayo, pamoja na sherehe kubwa na za aina yake kuwapongeza mabingwa hao mwishoni mwa wiki iliyopita, ni wakati sasa wa wawakilishi wetu hao kuanza maandalizi ili waweze kutuwakilisha vyema.
Ieleweke kuwa, mashindano hayo ni magumu na hayahitaji maandalizi ya zimamoto, bali mikakati madhubuti ndiyo dira ya mafanikio huko twendako.
Bila shaka, maandalizi hayo ni lazima yajumuishe mechi za kujipima nguvu dhidi ya timu kubwa za ndani na nje na ambazo zina uzoefu wa mashindano makubwa kama hayo.
Huu si wakati wa kulala na kusubiri kujua timu watakazopangiwa nazo ndipo waanze kupiga mbio, bali ni vyema viongozi wa timu hizo zikae na kupanga programu nzuri, na pia kutafuta njia ya kupata fedha kwa ajili ya kugharamia ushiriki wao.
Wazanzibari tumechoka kuziona timu zetu zinazotuwakilisha kimataifa, kuwa washindikizaji wa maisha na kuishia raundi za kwanza kwenye michuano ya Afrika.
Sasa tunataka kuona aibu hiyo inafutwa na kupiga hatua kubwa mbele ili nasi tuingie kwenye chati ya nchi zinazotisha katika medani ya soka.
Mafanikio katika jambo lolote lile, hayaji kwa njia za mkato, bali ni lazima kuwe na mipango imara na yenye kutekelezeka ikiwemo kuweka kambi muda wa kuingia mashindano utapokaribia.
Pia ni lazima tujiulize huwaje nchi za wenzetu zikiwemo majirani wa karibu, zinaweza kufanya vizuri na sisi daima tumekuwa ngazi kwao ya kupandia na kufika kileleni.
Viongozi wengi wa michezo hapa Zanzibar wamekuwa na mawazo mgando, ambapo wamejenga imani kuwa ‘kamati za ufundi’ ndizo zenye umuhimu wa kuleta ushindi michezoni.
Ninaposema ‘kamati za ufundi’ usidhani ni zile za kitaalamu zinazohusisha makocha na madaktari, bali ni hizo zinazotumika kusaka ushindi kwa kutumia njia za uchawi au wengine huita ndumba.
Katika ulimwengu huu mambo huendeshwa kisayansi zaidi, imani za kishirikina katika michezo hazina nafasi tena na lazima mkazo uwekwe katika kuziandaa timu na kuzijengea uwezo kwa kuzipatia mahitaji yote ya lazima badala ya kunufaisha wachawi bila tija yoyote.
Haifai timu kutumbukiza fedha nyingi kwa wachawi huku wachezaji wakilia njaa na hivyo kuporomoka viwango na moyo wa kuzitumikia timu zao.
Kwa kuwa tayari timu zitakazotuwakilisha kwenye michuano ya kimataifa zimeshajulikana, ni muda muafaka sasa kuanza kujipanga, na hakutakuwa na sababu ya kutafuta viongozi, vya kukosa muda wa kutosha wa kujiandaa.
Kwa kawaida, mashindano ya Afrika huanza mwezi wa Februari, na ile ya Kagame huchezwa katikati ya mwaka, hivyo tunao muda wa kutosha kujenga vikosi imara vitavyotuwakilisha vizuri, tena ibaki kushindwa kimchezo tu.
Aidha, wachezaji nao hawana budi kuepusha mambo ya anasa ambazo zitachangia kushusha uwezo wao na kusababisha kufanya vibaya.
Ni lazima nao wawekwe darasani kupigwa msasa wa kisaikolojia ili kuwafanya waelekeze akili zao kwenye kazi ngumu iliyo mbele yao , badala ya kutarajia ushindi usioandaliwa mazingira mazuri.
Viongozi wa timu au hata wa kisiasa nao wanahusika pia kuzisaidia timu, kwani wamekuwa na tabia ya kutoa ahadi kwamba timu zikishinda watatoa motisha.
Ndugu zangu, motisha haitolewi wakati timu zikiwa uwanjani kucheza mechi husika bali huhitajika zikiwa kwenye maadalizi kwani wakati huo ndipo zinapokuwa zinahitaji msukumo na motisha ya hali ya juu ili kuhamasisha ushindi.
Nalisema hili kutokana na kumbukumbu za nyuma ambapo imewahi kutokea katika uwanja wa Amaan baadhi ya viongozi wa vyama vya siasa kunadi ahadi za fedha wakati mchezo ukiendelea, huku timu za nyumbani zikiwa zimeshafungwa.
Ahadi kama hizo hazisaidii kitu kwani huwa sawa na kumpa dawa mgonjwa aliye katika sakaratul mauti, akikaribia kukata roho.
Aidha, haitakuwa vyema, kuja kusikia klabu zetu zikitangaza kushiriki mashindano hayo kwa sababu ya ukata wa fedha kama ilivyotokea hivi karibuni pale Super Falcon ilipojiondoa kwenye ligi ya mabingwa Afrika.
Ili kuepuka hali hiyo, nadhani huu wakati mzuri pia kwa Kamati ya Kuendeleza Michezo Zanzibar (KUMIZA), ianze harakati sasa kutafuta namna ya kuzisaidia klabu zetu hizo.

No comments:

Post a Comment

lisungu_chisara@yahoo.com

TUTUMIE HABARI YOYOTE YA MICHEZO, BURUDANI TUTAZICHAPISHA

TANGAZA KWA MFUMO HUU

MAHUDHURIO YA WASOMAJI KIMATAIFA

free counters

Followers