HABARI MPENZI MWANAMICHEZO KARIBU KATIKA KURASA HII MAHSUSI KWA HABARI ZA MICHEZO PIA UNAWEZA KUTANGAZA BIASHARA YAKO HAPA KWA BEI NAFUU ZAIDI KWA MUDA MREFU ZAIDI WASILIANA NASI KWA NAMBA +255713 15 33 48

28 October 2013

NAKUKABIDHI KATIBA ILINDE

Jamal Emil Malinzi ndiye Rais mpya wa Shirikisho la Mpira wa Miguu Tanzania (TFF) baada ya kuibuka kidedea katika uchaguzi mkuu wa shirikisho hilo kwa kupata kura 73 kati ya kura 126 zilizopigwa, dhidi ya mpinzania wake Athumani Nyamlani aliyepata kura 52 kwenye kinyang'anyiro hicho kilichohitimishwa usiku wa kuamkia leo katika jengo la NSSF la Waterfront jijini Dar es salaam.


Malinzi ambaye pia ni mwenyekiti wa chama cha soka cha mkoa wa Kagera ameshinda uchaguzi huo ikiwa ni mara yake ya pili kugombea baada ya kushindwa na Rais wa zamani wa TFF Leodgar Chillah tenga mwaka 2008.Nafasi ya Makamu wa Rais imenyakuliwa na Wallace Kiria aliyemshinda Ramadhani Nasib kwa kura 67 dhidi ya 52, wakati mgombea mwingine katika nafasi hiyo Imani Mahugila Madega kapata kuta 6.

Katika nafasi za Ujumbe; Kanda ya 13; kiungo wa zamani wa Simba SC Wilfred Kidau amepata kura 60 na kuwashinda Muhsin Said kura 50, Omar Abdulkadir kura 10 na Alex Kabuzelia kura nne.

Kanda 12; Khalid Mohamed Abdallah amepata kura 69 na kumshinda Davies Mosha aliyepata kura 54.


Kanda ya 11 Geoffrey Nyange ‘Kaburu’ amepata kura 78 na kuwashinda Riziki Majala kura tano, Twahir Njoki kura mbili, Juma Pinto kura 26 na Farid Mbaraka kura 14, Kanda ya 10 ameshinda Hussein Mwamba aliyepata kura 63, huku Charles Komba akipata nne na Stewart Nasima 58.


Kanda ya tisa Othman Kambi aliyepata kura 84 yeye amewashinda Francis Bulame kura 30, wakati James Mhagama aliyepata 93 amemshinda Zafarani Damoda aliyepata kura 11 na Kanda ya nane, Ngube Kiondo amepata kura 73 amemshinda Ayoub Nyaulingo kura 52.

Kanda ya Tano, Ahmed Iddi Mgoyi aliyepata kura 92 amemshinda Yussuf Kitumbo aliyepata kura 34, wakati Kanda Omar Walii Ali amepata kura 53 dhidi ya 19 za Ally Mtumwa.


Eley Mbise amepata kura 51 dhidi ya 53 kura 57 za Lamanda Swai.
Mbasha Matutu aliyepata kura 63, amembwaga Vesastis Ligano aliyepata kura 61, wakati Vedastus Lufano aliyepata kura 51, amewashinda Jumbe Odesa Magati kura 11, Mugisha Galibona kura 24 na Samuel Nyalla kura 39 na Kanda namba moja, Karilo Samson hakuwa na mpizani akapita moja kwa moja.


Rais mpya wa TFF Jamal Malinzi akiwa na Dream Team yake baada ya uchaguzi



Rais Mstaafu wa TFF LEodegar Chilla Tenga akimkabidhi mikoba Rais Mpya Jamali Malinzi akkisaidiwa na katibu mkuu Angetille Osiah.

Rais wa Shirikisho la Mpira wa miguu nchini aliyemaliza muda wake,Leodger Tenga (kushoto) akimkabidhi Mpira Rais Mpya wa shirikisho hilo,Jamal Malinzi mara baada ya kutangazwa mshindi katika Uchaguzi uliofanyika jana na kumalizika usiku wa kuamkia leo,ambapo alimshinda mpinzani wake,Athuman Nyamlani kwa kura 73.uchaguzi huo ulifanyika katika ukumbi wa Mikutano wa Water Front jijini Dar es salaam.Katika uchaguzi huo nafasi ya Umakamu wa Rais ilichukuliwa na Walace Karia ambaye alifanikiwa kuwagaragaraza wapinzani wake Imani Madega na Ramadhan Nassib.


Rais Mpya wa Shirikisho la Mpira wa miguu nchini,Jamal Malinzi akizungumza machache na Wajumbe wa Uchaguzi huo mara baada ya kutangazwa Mshindi wa nafasi ya Urais wa TFF,usiku wa kuamkia leo kwenye Ukumbi wa Mikutano wa Water Front,jijini Dar es Salaam.Kulia ni Makamu Mpya wa Rais wa TFF,Walace Karia.

Rais Mpya wa Shirikisho la Mpira wa miguu nchini,Jamal Malinzi akipongezana na Makamu Mpya wa Rais wa TFF,Walace Karia mara baada ya kuibuka Kidedea.



.Picha na FullShangwe Blog via MICHUZIBLOG

25 October 2013

TUNAFURAHI KUSIKIA AJENDA- TENGA


Rais wa Shirikisho la Mpira wa Miguu Tanzania (TFF) anayemaliza muda wake, Leodegar Tenga amesema amefurahishwa na jinsi kampeni za uchaguzi zinazokwenda kutoka na ukweli kuwa wagombea wamekuwa wakielezea kile wanachotaka kuufanyia mpira wa miguu.

Akizungumza na waandishi wa habari kwenye ofisi za TFF leo mchana, Rais Tenga ambaye pia ni mjumbe wa Kamati ya Utendaji ya Shirikisho la Mpira wa Miguu Afrika (CAF) amesema Watanzania wanataka kusikia ajenda za wagombea.

“Ombi langu ni kwamba kampeni zimeanza vizuri, watu wanazungumza hoja zaidi. Ni jukumu la wajumbe kupima na kufanya uamuzi. Kwangu mimi nimejitayarisha kumkabidhi Katiba, Rais mpya wa TFF,” amesema.

Tenga ambaye pia ni Mwenyekiti wa Baraza la Vyama vya Mpira wa Miguu Afrika Mashariki na Kati (CECAFA) amesema kazi kubwa iliyofanywa na uongozi wake ni kujenga taasisi (TFF) pamoja na kuweka mifumo (structure) inayoainisha majukumu ya kila mmoja.

“Ajenda yetu wakati tunaingia madarakani mwaka 2005 ilikuwa ni kujenga taasisi. Tayari taasisi ipo, sasa mtazamo uwe kuushughulia mpira wa miguu wenyewe,” amesema.

Mkutano Mkuu wa TFF unafanyika kesho kwenye ukumbi wa mikutano wa NSSF Waterfront, na tayari wajumbe wa mkutano huo ambao pia utakuwa na ajenda ya uchaguzi siku inayofuata wameshawasili jijini Dar es Salaam.

Wawakilishi kutoka Shirikisho la Kimataifa la Mpira wa Miguu (FIFA), Ashford Mamelodi ambaye ni Ofisa Maendeleo wa kanda hii, Magdi Shams El Din ambaye ni mjumbe wa Kamati ya Utendaji ya CAF na Rais wa Chama cha Mpira wa Miguu Zanzibar (ZFA) ni miongoni mwa wageni watakaohudhuria mkutano huo.

Yahya Juma AUKWA UENYEKITI TPL BOARD




Hamad Yahya Juma wa Mtibwa Sugar ndiye Mwenyekiti wa kwanza wa Bodi ya Ligi Tanzania (Tanzania Professional League- TPL Board) baada ya kushinda katika uchaguzi uliofanyika leo mchana (Oktoba 25 mwaka huu) kwenye ukumbi wa mikutano uliopo Golden Jubilee Tower, Dar es Salaam.

Juma ambaye hakuwa na mpinzani alipata kura zote kumi za ndiyo zilizopigwa na klabu za Ligi Kuu zilizohudhuria mkutano huo. Klabu ambazo hazikuhudhuria uchaguzi huo ni JKT Ruvu, Mgambo Shooting, Coastal Union na Rhino Rangers.

Naye Said Muhammad Said Abeid ambaye pia hakuwa na mpinzani amechaguliwa kuwa Makamu Mwenyekiti kwa kupata kura zote za ndiyo.

Kwa upande wa wajumbe wawili wa Kamati ya Uendeshaji, wote Kazimoto Miraji Muzo wa Pamba na Khatib Omari Mwindadi wa Mwadui wameshinda kwa kura zilizopigwa na klabu za Ligi Daraja la Kwanza (FDL).

Muzo alipata kura 15 za ndiyo wakati mbili zikimkataa, huku Mwindadi akipata kura 16 na moja ilimkataa. Klabu za FDL ambazo hazikuhudhuria uchaguzi huo ni Transit Camp, Burkina Faso, Polisi Mara, Stand United, Toto Africans, Polisi Tabora na Kanembwa JKT.

23 October 2013

SOMA WASIFU WA JAMALI MALINZI JE ANAFAA KUWA RAIS WA TFF


UCHAGUZI WA SHIRIKISHO LA MPIRA WA MIGUU TANZANIA (TFF) 2013
ILANI YANGU YA UCHAGUZI
Utangulizi
Ndugu zangu,
Nianze kwa kumshukuru Mwenyezi Mungu mwingi wa Rehema aliyetulinda na kutuwezesha kufika
hapa tulipo.
Tarehe 19 Novemba 2009 Rais Jakaya Mrisho Kikwete wakati anazindua ziara ya Kombe la FIFA la
dunia uwanja wa Taifa, Dar Es Salaam pamoja na mambo mengine alisema, namnukuu:
‘‘Kwa Watanzania wenzangu tuichukulie ziara ya Kombe la Dunia nchini mwetu
kama ni changamoto kubwa kwetu inayotutaka tufanye vizuri zaidi katika soka ili
tulingane na heshima hii tuliyopewa. Hasa ni changamoto kwa viongozi wa soka wa
ngazi zote pamoja na wachezaji na wapenzi wa mpira wa miguu nchini. Kuja kwa
kombe hili ni deni kwetu na kulilipa kwetu sisi ni kuzinduka, tuendeleze kiwango
chetu cha soka nchini ili na sisi siku moja TUSHIRIKI FAINALI ZA KOMBE
HILI (msisitizo ni wa kwangu). Hili jambo linawezekana. Wapo wenzetu Afrika
wameweza, kwa nini sisi tusiweze? Wao ni watu kama sisi, maadam wameweza na
sisi tutaweza.
Lakini ili tuweze hatuna budi kuiga mfano hususani waliyofanya wenzetu na
wanayoendelea kufanya kuendeleza mpira wa miguu. Twende tukajifunze kutoka
kwao. Lakini hata kabla ya kwenda huko, yapo mambo hatuna budi kuyafanya.
Naomba nitaje baadhi yake:
1. Tuimarishe Uongozi, utendaji na uendeshaji wa vilabu vya mpira. Mchezaji
hufundishwa kucheza mpira katika Klabu yake. Hapo ndipo hufundishwa
maarifa ya kucheza mpira na vipaji kuendelezwa. Hebu tujiulize hali ya
vilabu vyetu vya soka ikoje. Je vinaongozwa vizuri? Vinaendeshwa vizuri?
Jibu tunalijua sote kuwa ni hapana. Lazima suala hili tulitafakari kwa makini
na kulipatia jawabu. Tukishindwa kupata jawabu muafaka na mambo
yakaachwa kuendelea yalivyo, mpaka mwisho wa dunia hatutakuwa tunasogea
popote.
2. Tupate walimu wenye uzoefu kufundisha timu zetu. Hii ndiyo njia ya uhakika
ya kukuza na kuendeleza vipaji na hivyo kupata wachezaji bora.
3. Tuwekeze katika kuibua na kuendeleza vipaji vya wachezaji toka umri mdogo.
Vilabu viwe na timu za watoto na vijana. TFF isaidie kuanzishwa kwa shule
za mchezo wa mpira wa miguu kwa watoto na vijana. Mashuleni wapatikane
walimu wa michezo walio wazuri kufundisha.
4. TFF ionekane zaidi ya ilivyo sasa katika mipango ya kuendeleza soka
mashuleni, vijijini, mitaani na vilabuni. TFF ikiwa na mipango na kuisimamia
na kuwabana wadau kuitekeleza itasaidia. Vinginevyo TFF itabakia
kusimamia Ligi Kuu, kutoa adhabu kwa wachezaji na kusimamia timu ya
Taifa. Hiyo haitoshi.’’
Mwisho wa kunukuu.
Ndugu zangu wajumbe wa Mkutano Mkuu wa TFF, wadau na wapenzi wa mpira wa Miguu Tanzania
tujiulize kuanzia kipindi hicho cha 2009 hadi leo hii katika haya maagizo ya Mheshimiwa Rais Jakaya
Mrisho Kikwete tumetekeleza yapi zaidi ya kuwa wasindikizaji katika medani ya kimataifa? Kipindi
chote cha miaka minane iliyopita Serikali imetoa sapoti kubwa katika sekta ya mpira wa miguu kwa
kulipia walimu wa timu za Taifa na kuhimiza makampuni kama NMB,Serengeti Breweries,Airtel,Coca
Cola na sasa Tanzania Breweries kudhamini timu zetu za taifa na mashindano mbali mbali,matunda
yake yako wapi? Ndo kwanza tunazidi kuporomoka kwenye viwango vya FIFA. Iweje miaka ya
nyuma timu zetu za Taifa zilifanya vizuri wakati zinaweka kambi Salvation Army, leo zinakaa hotel za
nyota tatu mafanikio mbona hatuyaoni? Kama TFF imeondolewa gharama za kulipa makocha,kuweka
timu kambini,kununua vifaa vya timu,dawa,posho,malazi pamoja na usafiri wa timu iweje leo TFF
ishindwe kutumia vyanzo vyake vya mapato zikiwemo fedha toka FIFA na CAF kwa ajili ya
kuanzisha na kuendeleza programmu ya vijana ya kitaifa? Kwa mujibu wa mtandao wa FIFA kati ya
mwaka 2008 na 2012 TFF imepokea toka FIFA msaada wa jumla ya dola za kimarekani milioni moja
na lake nane na nusu (yapata shilingi bilioni tatu za kitanzania), hizi fedha zimefanyia nini? Kwa nini
timu za vijana hazina udhamini? Ipi timu yetu ya taifa iwe ya wanaume wakubwa (senior team) ,
wanawake au za vijana inayoweza leo hii kujivunia mafanikio? Iko wapi ligi ya wanawake? Katika
hili tusilaumu Chama cha mpira cha wanawake, wakiwezeshwa wanaweza.Tutapataje timu mahiri ya
Twiga stars bila ligi ya wanawake? Katika ngazi ya klabu, hasa zinazoendeshwa kwa mfumo wa
kijamii kama Toto Africa, Coastal Union, Yanga, Simba,Mbeya City n.k. hadi leo hii pamoja na
rasilimali za vilabu hivi ni klabu ipi imeweza kusimamia na kujiendesha yenyewe tokana na vyanzo
vyake yenyewe? Tuendelee kujiuliza:
 Ni walimu wangapi wa mpira tumewaendeleza kufikia kiwango cha kukabidhiwa majukumu ya
kufundisha Taifa Stars. Fursa za mafunzo tunazopewa na FIFA na CAF tunazitumiaje? Je
tumeweza kuwa na angalau kocha mmoja anayefundisha mpira nje ya nchi kama ilivyo kwa
akina Sam Timbe ( wa Uganda), James Sianga ( wa Kenya) Jack Chamangwana ( wa Malawi)
na wengine ambao waliweza kufundisha mpira Tanzania kwa ufanisi?
 Ni refa gani tumemuendeleza akafikia kiwango cha kuchezesha mashindano ya fainali za dunia
au AFCON au Klabu bingwa ya Africa? Refa wa mwisho kuchezesha fainali za Mataifa Africa
(AFCON) ni Omar Abdulkadir huko Burkina Faso mwaka 1998.
 Ni program ipi ya vijana ya kuibua vipaji na kuviendeleza tuliyo nayo? Wale vijana wa Copa
Cocacola 2007 waliopelekwa kwa mbwembwe Brazil waliishia wapi? Tuna rekodi
zao?Tunajua wako wapi na wanafanya nini? Na hawa walioshinda majuzi Afrika Airtel Rising
Stars tumewatangenezea program gani ya maendeleo?
 Tunaelewa matatizo ya vilabu vya mpira hususani uhaba wa vifaa na pesa za uendeshaji, je
vilabu vyetu TFF inavisaidiaje katika kuendeleza programu zao za vijana?Au kazi yetu ni kudai
kila klabu iwe na timu ya under 20 bila kujali gharama za uendeshaji wa timu hizi?
 TFF hadi sasa imebuni, kusimamia na kutekeleza program endelevu ipi ya kuendeleza soka
mashuleni, vijijini, mitaani au vilabuni? Au mpaka tusubiri Airtel rising Star na Copa
Cocacola? Siku wakubwa hawa wakisusa itakuwaje?
 Ziko wapi juhudi za kuhimiza upatikani wa vifaa vya kufundishia mpira watoto (kama mipira
size 3/4) pamoja na kuimarisha miradi ya kuendeleza vijana ?
 Hivi timu zetu za Taifa zinatumia mfumo upi wa uchezaji? Au kila kocha wa taifa tunayemleta
anakuja na mfumo wake? Wenzetu wameweza kubuni mifumo ya uchezaji ya timu zao za
Taifa na wameushirikisha katika mfumo wa ufundishaji wa watoto. Lini Mwalimu wetu wa
Taifa alikaa na walimu wa vilabu (angalau vya Premier League) ili kujadili ufundishwaji wa
mpira nchini, hii ikiwa ni pamoja na kujadili masuala yahusuyo mbinu, lishe, huduma za afya
na ukakamavu wa mwili? Hivi mchezaji akitoka katika klabu yake ambako amezoea kula dona
na maharage ukampeleka kambi ya Timu ya Taifa akapewa prawns ,kuku na samaki kwa siku
nne za kambi itamsaidia kumbadili siha? Ng’ombe hanenepeshwi siku ya mnada.Uratibu wa
programu za vilabu ni muhimu.
 Raha ya mpira ni kelele na hoi hoi za mashabiki. Wataalam wa mpira wanasema umoja wa
mashabiki wa mpira ni sawa na mchezaji wa 12 uwanjani. Zipo timu ambazo kihistoria
zilikuwa ni za kijamii na zilihamasisha sana ligi ya Taifa, na kuiongeza hamasa na
ushindani,Mbeya City ni mashahidi. Leo hii ziko wapi timu kama Ushirika ya Moshi, Bandari
ya Mtwara, Kariakoo Lindi, Balimi Bukoba, Reli Kiboko ya vigogo, Kahama United, Mirambo
ya Tabora, Tukuyu Stars, Nyota Korogwe, African Sports ya Tanga,Ujenzi Rukwa,Mji
Mpwapwa n.k. TFF imefanya juhudi gani kufufua ushidani huu kwa kushirikiana na vyama
vya Mikoa na Wilaya?
 Wapo wachezaji wastaafu waliojitolea kwa moyo mmoja kuiletea heshima nchi yetu. Leo hii
tunasikia kina Alfonce Modest na Jellah Mtagwa wanalalamika hawana msaada, na hao ndio
wale waliojitolea hadharani kutoa kilio chao. TFF hadi leo hii imewahi kuandaa mpango gani
endelevu wa kuwasaidia wachezaji wastaafu? Shirikisho la mpira barani Afrika CAF
wameanzisha ISSA HAYATOU TRUST FUND kusaidia wachezaji wastaafu waishio katika
mazingira magumu,sisi tumechukua hatua gani katika hili?
 Iweje mpake leo hakuna mashindano yoyote ya wanawake ya kitaifa yawe ya ligi au ya
mtoano,angalau kwa ngazi ya kanda ? TFF itawezaje kuibua vipaji vipya vya timu ya taifa ya
wanawake TWIGA Stars bila mashindano ya aina hii?
 Vilabu vya mpira, hususani vya Ligi Kuu, vimegeuka kuwa kisima cha watu kuchota fedha.
Haiyumkiniki vilabu ambavyo vinaweka timu kambini, kuihudumai kuanzia malazi, posho,
vifaa, madawa na usafiri mwisho wa mechi jumla ya pesa wanayopewa inakuwa chini ya nusu
ya mapato yote ya mechi. Hayo maendeleo ya mpira ambayo yametakiwa yaanzie ngazi ya
vilabu yatapatikanaje? Vilabu vimegeuka vitega uchumi vya watu wengine wakati vyenyewe
vinataabika na kujiendesha kwa mateso makubwa.
Ya kusema ni mengi, kwa leo tuishie hapa.
Nini matokeo ya hali hii? Takwimu hazidanganyi. Matokeo ya hali hii ni timu za Taifa kushuka
viwango katika orodha ya FIFA siku hadi siku. Viwango vya timu za taifa vinapimwa kwa kuangalia
uwiano wa matokeo ya timu ya wakubwa (senior) pamoja na yale ya timu nyingine za vijana za nchi
husika. Miaka ya mwanzo ya tisini tulishawahi kupanda hadi nafasi ya 65, leo hii kila kukicha tuko
kwenye 120.Kuporomoka huku kutaendelea hadi lini?
Ndugu zangu, tujiulize wapi tumetoka, tuko wapi na tunataka kuelekea wapi? Jibu ni rahisi, kama
alivyoagiza Mh Rais Kikwete,tujipange upya, tubuni mkakati wa uendelezaji wa mpira, tuandae
program endelevu yenye malengo yanayopimika na kwa pamoja tukishirikiana na Serikali, FIFA
CAF na CECAFA,Halmashauri, Taasisi zisizo za kiserikali, Sekta binafsi, Vyombo vya habari na
wadau wengine wote wa mpira wa miguu tutaweza kufanya vizuri na kuifanya Tanzania isifike
duniani kote. Katika kutimiza azma hii sharti tuanzie kwa kuleta mabadiliko ya uongozi wa juu wa
TFF, tupate kiongozi ambaye sio sehemu ya mapungufu ya TFF,hakuna njia ya mkato.Mimi Jamal
Emil Malinzi,nimejipima na ninaamini nina uwezo wa kutosha wa kubuni, kuratibu na
kusimamia mabadiliko haya nikiwa Rais wa TFF.
Ndugu zangu, siku zote si vyema kukosoa bila kueleza njia mbadala ya kufuata ili kutatua tatizo. Hapa
tunazungumzia mpira wa miguu na namna ya kuunasua toka kwenye janga la kushuka kiwango na
timu zetu za Taifa kuendelea kugeuzwa kichwa cha mwenda wazimu ambacho hadi majuzi vibonde
Gambia wamejifunzia kunyoa.
Ili tuweze kuukwamua mpira wetu ni vyema tukakumbushana kuwa ili mpira uendelee unahitaji vitu
vinne:
1. Vipaji;
2. Walimu;
3. Vifaa;
4. Viwanja
1. Vipaji
Tanzania ni nchi yenye watu zaidi ya milioni 44. Nchi ya Cape Verde yenye watu 500,000 tu
imeweza pamoja na uchache wake kuvumbua vijana 11 ambao wameweza kuifikisha nchi yao
fainali za Africa 2013 Afrika Kusini na majuzi nusura waende kombe la dunia kama sio tatizo
la utunzaji kumbukumbu. Sayansi ya uibuaji vipaji (scouting) ni muhimu na si kila mtu
anaijua. Watafutwe wanaoijua, watufanyie kazi ya kutuibulia vipaji vipya, na katika hili ni
sharti mpira wa ushindani uchezwe nchini kote ili vipaji vionekane.
2. Walimu
Mpira ni sayansi,mpira ni taaluma. Kipaji bila mwalimu wa kukiendeleza ni bure. Vijana
mpira wanaanza kuucheza wakiwa wadogo hususani wakiwa shule za msingi. Huko ndiko
Taifa linahitaji kusambaza walimu wenye taaluma ya kufundisha mpira ngazi ya awali.
Wakishakuzwa kimpira ni lazima wawepo walimu wa kutosha kuwaendeleza ngazi ya
wakubwa na Taifa. Leo hii Uingereza ina walimu 1100 wenye leseni daraja A,Ujerumani wapo
5500 na Hispania 12,000,Tanzania tunaye mmoja tu,kwa mtaji huu tutafika kweli?Kwa mujibu
wa ripoti ya TFF nchi nzima ya Tanzania ina walimu wa mpira wa madaraja yote elfu mbili tu
na mia tano kati yao wako Dar es salaam. Hawa walimu 2000 ndio wanategemewa
wawafundishe mpira vijana wa Kitanzania zaidi ya milioni kumi walio katika umri wa
kufundishwa mpira!
3. Vifaa
Wachezaji, walimu wa mpira, madaktari na waamuzi wote wanahitaji vifaa vya msingi ili
mpira uchezwe. Nchini mwetu vijana walio wengi wanacheza pekupeku, jezi ni upande mmoja
kucheza kifua wazi, mpira ni wa kuviringisha matambara, refa anavaa suruali, filimbi ni mluzi,
magoli hayana nyavu, n.k. Hii ndiyo hali halisi ya uchezwaji wa mpira maeneo mengi
Tanzania hasa vijijini ambako ndiko kunapaswa kuwa chimbuko kubwa la vipaji.
Gharama za vifaa vya michezo ziko juu mno, mfano mpira mzuri unaofaa kuchezewa kwenye
ardhi ngumu (rough surface) bei yake ni shilingi laki tatu, shule ipi ya msingi itaweza
kuununua huu mpira? Kuna baadhi ya vyombo vya habari majuzi viliripoti kuwa kuna
mchezaji alifunga hat trick ngazi ya Ligi Taifa akanyimwa mpira kisa ni wa thamani kubwa.
Mamlaka husika, hasa za kodi zinapaswa kuliangalia hili, ili upatikane unafuu katika bei za
vifaa vya michezo maana karibia vyote vinaagizwa toka nje. Lakini pia vifaa vya michezo vya
misaada vinavyopatikana kutokana na miradi mbalimbali ya TFF ni juu ya TFF kuhakikisha
vinafikishwa vijijini pia kupitia vyama vya mikoa na wilaya.
4. Viwanja
Wilayani Ngara mkoani Kagera kuna uwanja wa mpira unaitwa ‘’Uwanja wa Changarawe’’ na ni
kweli uwanja huo umejaa changarawe. Beki akikaba kwa mtindo wa kuteleza ardhini ‘sliding tackle’
basi nyama ya paja anaiacha pale chini. Hii ndiyo hali halisi ya viwanja vyetu vingi nchini, kama vipo
ni vibovu sana maana maeneo mengi viwanja vya mpira hakuna vimechukuliwa na wajanja wachache
na kugeuzwa makazi na majengo ya biashara. Tunahitaji viwanja vyenye ubora ili vijana wetu
wafundishwe mpira wa kisasa kwa ufanisi, mpira wa kupiga pasi ya chini. TFF kwa kushirikiana na
vyama vya Mikoa na Wilaya sharti wawe mstari wa mbele katika kulipigania hili.
AHADI YANGU
Endapo nitachaguliwa kuwa Rais wa TFF, kwa kushirikiana na viongozi wote wa TFF kuanzia ngazi
ya vilabu, Wilaya, Mikoa na Kamati ya Utendaji Taifa na kwa kuhusisha kwa karibu Vyama vya
kimataifa vya FIFA na CAF, Serikali, Halmashauri,Taasisi zisizo za kiserikali, Vyombo vya habari,
Sekta binafsi, Mashirika ya umma na wadau wa mpira wa miguu Tanzania ninaahidi kuenzi mafanikio
ya awamu inayomaliza muda wake , kustawisha utulivu katika uendeshaji wa mpira, na kufanya
jitihada za kubuni, kuboresha na kustawisha maendeleo ya mpira wa miguu Tanzania. Jitihada kubwa
zitawekwa kwenye maeneo makuu yafuatayo:
1. Ufundi (Technical)
1.1 Muundo wa Idara ya Ufundi
Katiba ya TFF imeainisha wazi kuwa TFF ndiye msimamizi mkuu wa mpira wa miguu
Tanzania, hivyo jukumu la kuleta maendeleo ya mchezo huu kwa kiasi kikubwa linaiangukia
TFF.Ni kwa msingi huu basi asilimia kubwa ya rasilimali za TFF lazima iwekezwe katika
kuleta maendeleo ya mpira. Kwa mfumo wetu wa uendeshaji, kichocheo kikuu cha maendeleo
ya mpira ni idara ya ufundi ya TFF. Hivyo idara hii ya ufundi inapaswa kuwa ndiyo idara
mama ya TFF ambayo inapaswa kuongoza kwa matumizi ya fedha, idadi ya waajiriwa na
matumizi ya rasilimali nyingine za TFF . Kwa sasa pale TFF hali sivyo ilivyo. Iwapo
nitachaguliwa nitapendekeza jukumu la kwanza la Kamati ya utendaji liwe ni kurekebisha na
kuboresha mfumo wa uendeshaji wa idara ya ufundi. Nitapendekeza idara ya ufundi iendelee
kuongozwa na Mkurugenzi wa Ufundi na chini yake awe na wakurugenzi wasaidizi wa vitengo
watatu Mkurugenzi Msaidizi (ufundi), Mkurugenzi Msaidizi (Elimu na Mafunzo) ambaye kwa
sasa anaitwa Education officer, na Mkurugenzi Msaidizi (Maendeleo ya mpira).
Kitengo cha Ufundi kitahusika na kubuni na kusimamia shughuli zote zinazohusu maendeleo
ya Timu za Taifa kuanzia za wakubwa hadi za vijana. Hii itakuwa ni pamoja na kuandaa
mitaala ya taifa (national football curriculum) ya ufundishaji wa mpira Tanzania kuanzia umri
wa miaka mitano hadi watu wazima. Walimu wa Timu za Taifa wataripoti kwake.
Kitengo cha Elimu na Mafunzo kitahusika na kubuni na kuratibu kozi zote na mafunzo yote
yanayohusiana na mpira kama vile kozi za Marefa, Makocha, Madaktari, Makamisaa,
Watawala, Waandishi wa Habari za Michezo, n.k.
Kitengo cha Maendeleo ya mpira kitahusika na kubuni,kuratibu na kusimamia mpango wa
maendeleo ya vijana (grassroot) na kutafuta vipaji (scouting). Kitengo hiki kitafanya kazi kwa
kushirikiana kwa ukaribu na idara za Serikali hasa idara za Elimu,Vijana na TAMISEMI,
Halmashauri,Mashirika ya umma,Sekta binafsi pamoja na Taasisi nyingine za kijamii.
Wakuu wa vitengo hivi wataajiriwa kwa kufuata vigezo makini na bila upendeleo wala
kujuana.
1.2 Ujenzi wa Kituo cha Mpira (Football Centre of excellency)
Hiki ni Kituo Maalum cha mafunzo ya mpira wa miguu. Katika kituo hiki kunakuwa na kila
aina ya miundo mbinu, viwanja vya kufundishia mpira, vituo vya tiba,madarasa ,maabara za
utafiti,hosteli n.k Kituo hiki pia kinakuwa ndio sehemu kuu ya kuweka kambi za timu za Taifa
na kutoa mafunzo ya ufundi yakiwemo ya ukocha, urefa, utawala na tiba. Wenzetu wa Senegal
na Ethiopia kwa kushirikiana na Shirikisho la Mpira Africa CAF wameweza kujenga vituo hivi
na matokeo yake tunayaona.Cameroon pia wana kituo hiki.
Pamoja na gharama zake kuwa kubwa, cha muhimu hapa ni kuweka nia, kutafuta ardhi kwa
kushirikiana na Serikali na kuanza ujenzi taratibu.Kwa kuwa klabu ya Sunderland ya Uingereza
na kampuni ya kufua umeme ya Symbion wameonyesha nia ya kushirikiana naSerikali kujenga
kituo cha michezo itakuwa vyema iwapo TFF itashirikiana na taasisi hizi muhimu ili kufikia
azma ya kujenga kituo hiki cha kisasa. Iwapo nitachaguliwa nitasimamia uanzishwaji wa mradi
huu muhimu ikiwa ni sehemu ya mkakati wa kulikomboa soka letu.
Aidha uwanja wa Karume yalipo makao makuu ya TFF utazungushiwa jukwaa ili mechi
ambazo sio kubwa zifanyike pale, Hii itaiongezea TFF mapato na vilabu pia.
1.3 Timu Kupanda Daraja
Ili kuongeza ushindani na kupanua mpira uchezwe kona zote za nchini ( to spread the game)
,mtindo wa kucheza kikanda ili kupata timu za kupanda daraja kuu utakuwa ni wa kudumu na
utaimarishwa kwa kutafutiwa udhamini na kuboreshwa viwanja kwa kushirikiana na wamiliki
wa viwanja hivyo. Usimamizi wa mashindano ngazi hii utaimarishwa na kusimamiwa kwa
karibu zaidi ili timu itakayopanda daraja iwe imepanda kwa haki na hivyo kuleta ushindani
Ligi Kuu.
Hata hivyo waraka uliotolewa na TFF ukiagiza mikoa ichezeshe ligi ili kupata bingwa wa
mkoa utafutwa kwa sababu hautekelezeki kutokana na hali ya uchumi na uhalisia wa jiografia
ya mikoa ya Tanzania. Mathalani Mkoa wa Mtwara ukichezesha ligi ya mkoa (kwa maana ya
nyumbani na ugenini) ina maana bingwa wa Wilaya ya Masasi atasafiri vipi akacheze
Newala au Mkoani Lindi bingwa wa Liwale atasafiri vipi akacheze na bingwa wa Kilwa ,
Pwani bingwa wa Mafia atasafiri kwa gharama za nani akacheze Bagamoyo na wa Kibaha
akacheze Utete? Pamoja na nia njema ya TFF uhalisia hauruhusu. Kama Mwenyekiti wa chama
cha mpira mkoa wa Kagera nalijua hili, hakuna haja ya TFF kuwa inatoa maelekezo ambayo
hayatekelezeki, hasa ukizingatia kuwa TFF hakuna msaada wanaopeleka kusaidia mikoa na
wilaya ziandae mashindano yao.Vyama vya mikoa na wilaya viachwe viendelee kutumia
ubunifu wao kupata mabingwa wao kulingana na hali halisi ya mazingira yao.
1.4 Kuanzisha mashindano mapya na kufufua ya zamani
Wataalam wa kandanda wanasema kuwa ili mchezaji awe katika kiwango bora inabidi acheze
kwa mwaka kimashindano wastani wa mechi 40. Ligi yetu kuu,Vodacom premier
league,inatoa fursa kwa mchezaji kucheza michezo 26 kwa mwaka iwapo anapangwa kila
mechi.Hii haitoshi. Namna pekee ya kurekebisha hali hii ni kuongeza idadi ya mashindano kwa
mwaka.Hili litafanyika kwa kufufua kombe la Taifa (Taifa cup) na kuanzisha kombe la
shirikisho (kama FA cup ya Uingereza). Kombe la shirikisho litashirikisha timu zote nchini
kuanzia ngazi ya kata,tarafa,wilaya,mkoa hadi Taifa na bingwa wake atawakilisha nchi katika
kombe la shirikisho la Afrika CAF confederation cup (kama ilivyo Kenya kwa sasa).
1.5. Mpira wa Wanawake
Hadi sasa hatuna mfumo imara na unaoeleweka wa kuendeleza soka la kinamama. Mpira wa
wanawake umeanzia Wilaya ya Kinondoni, ukakulia Wilaya ya Kinondoni na umegotea
Wilaya ya Kinondoni ambako kuna timu zenye majina kama Mburahati Queens na Sayari
Queens. Mpira wa wanawake sharti usambae nchi nzima, na ili kufanikisha azma hii lazima
yaanzishwe mashindano ya kitaifa ya wanawake ikiwemo Ligi ya taifa ya wanawake. Hii
itaendana na juhudi za kuongeza makocha, waamuzi na makamisaa wanawake na kutafuta
udhamini kwa timu ya Taifa ya wanawake TWIGA STARS.
1.6 Maandalizi ya Vijana (Grassroot Programme)
Mpango endelevu wa maendeleo ya soka la vijana sharti uandaliwe, uratibiwe na kusimamiwa
kwa makini. Program madhubuti ya maendeleo ya mpira wa vijana lazima ibuniwe ,iratibiwe
na kusimamiwa kwa usatadi mkubwa.Mradi huu lazima ulenge ,kwa hatua,kufikia hatua ya
kuingiza timu zetu fainali za kombe la Afrika la vijana chini ya umri wa miaka 17 na 20,fainali
za olimpiki, fainali za Afrika wachezaji wa ndani CHAN,fainali za Afrika AFCON na mwisho
fainali za kombe la dunia.Hii itakuwa ni pamoja na kujiwekea utaratibu wa mzuri wa
kuhakikisha vijana wetu wanapata fursa ya kucheza mpira nje ya nchi ili kujiongezea
umahiri.Na hii ni kwa wanawake na wanaume.
Mpango huu ni lazima ushirikishe Serikali Kuu (hasa Wizara zenye dhamana ya Michezo,
Elimu na Halmashauri), Taasisi zisizo za kiserikali,mashirika ya umma,sekta binafsi na
TFF,CAF na FIFA. Ushirikishwaji wa Serikali na Halmashauri katika program hii ni muhimu
sana kwa kuwa ndio wasimamizi na wamiliki wa shule nyingi za msingi ambako ndiko vijana
wetu wanakoanzia kucheza mpira. Mpango kazi huu lazima uonyeshe:
1. Nini tunataka kufanikisha.
2. Utaratibu utakaotumika.
3. Nguvu kazi inayotakiwa na sifa zake.
4. Mwongozo wa kufuatilia kupima ufanisi wa programu.
5. Kupambanua gharama za mpango na taratibu za uchangiaji wake.
Hatua muhimu katika kufanikisha program hii zitakuwa ni:
-Kufundisha walimu wa walimu (instructors), hawa ndio watakuwa chachu ya kupata
walimu wa mpira mashuleni na mitaani.
-Walimu wa walimu (instructors) kufundisha walimu wa kutosha wa michezo mashuleni na
mitaani
-Kwa kushirikiana na wamiliki wa shule kuhakikisha viwanja vya kuchezea vinakidhi
viwango
-Kutafuta na kusambaza vifaa vya michezo mashuleni hasa mipira ya saizi muafaka kwa
mujibu wa viwango vya kimataifa.
-Kupata shule angalau moja kila mkoa itakayopokea watoto wenye vipaji maalum vya
kucheza mpira, pale ambapo wazazi hawataweza kuwalipia karo vijana hawa basi TFF
ihakikishe karo zao zinapatikana,huo ndio uwekezaji katika mpira.
-Kuandaa mashindano mbali mbali yatakayoshirikisha shule hizi ili kupata timu za taifa za
vijana wa umri mdogo wa kike na wa kiume.
-Kuhakikisha timu hizi za umri mdogo zinapata fursa ya kushiriki mashindano mbali mbali
ya kimataifa
- Kupata vikosi vizuri vya timu za taifa za vijana wa umri mdogo ambao watakua pamoja,
hao ndio watajenga msingi imara wa timu za Taifa za wakubwa kwa miaka ya baadae.
Itakuwa ni muhimu sana program hii iendane vizuri na ratiba nyingine za mashindano ya
kitaifa kama Umitashumta, Umisseta, Airtel rising star, Copa Coca Cola n.k.
- Kuanzisha mashindano ya kitaifa ya kombaini za shule za sekondari na ya kombaini za
vyuo vikuu. Wachezaji mahiri wa timu ya taifa kama Leodeger Chilla Tenga (Rais wa
TFF) na Leopold Tasso Mkebezi (meneja wa Taifa stars) waliibukia kwenye
mashindano kama haya Mkebezi akiwa beki wa kombaini ya sekondari za
Bukoba,Ihungo,Kahororo na Nyakato.
Aidha vituo vya michezo (sports academies) ambavyo tayari vipo vitatengenezewa utaratibu
wa usajili na kuwekewa utaribu wa kuviendesha.
Ili kuondoa ulalamishi wa vituo vya mafunzo (Academies) kulalamikia malipo pindi mchezaji
akisajiliwa timu kubwa, vituo vyote vya vijana vitasajiliwa na vijana wao wote wataingizwa
kwenye kumbukumbu za TFF (data base) kwa majina, saini na picha,hii itasaidia kuzuia sakata
kama la Mbwana Samata na klabu yake ya utotoni ya Mbagala maana kumbukumbu za TFF
zitakuwa ndio jibu la maswali yote.
1.7 Tiba
1. Tutaimarisha usalama uwanjani. Tutahimiza kila uwanja zinakochezwa mechi za ligi kuwe na
gari la wagonjwa na chumba cha dharura (emergency room).
Katika kuimarisha usalama tutahakikisha vifaa muhimu vya dharura kama vifaa vya hewa
(oxygen) na vifaa vya kushtua moyo (defibulator) vinakuwepo. Kwa sasa hapa Tanzania
uwanja pekee wenye vifaa hivi ni Uwanja wa Azam Chamazi. Ni jambo la kusikitisha kuona
hata uwanja mpya wa Taifa hauna chumba cha tiba dharura (emergency room) na kibaya zaidi
makato ya uwanja hayaendi kuanzisha huduma hii muhimu wakati viongozi mbalimbali wa
kitaifa wanahudhuria mechi uwanjani.
2. Mradi wa Goal Project wa FIFA unatoa pesa za tiba na mradi huu uliweka lengo la kuwa na
chumba cha kliniki pale uwanja wa Karume. Tutakifufua chumba hiki, tutakiwekea vifaa na
kuhakikisha huduma ya kliniki kwa wanamichezo iliyokuwa ikitolewa na madaktari kila
Jumapili inarudishwa. Posho itatafutwa ili madaktari watoa huduma angalau wapate nauli na
maji ya kunywa.
3. Wakati wa kujadiliana mikataba na wadhamini mbalimbali tutahakikisha kipengele cha
huduma za afya kinaingizwa katika mikataba. Udhamini utatafutwa kwa ajili ya vipimo vya
wachezaji kabla ya league (pre-league medical test) kama vile vipimo vya uvumilivu (Yo-Yo
test) na vipimo vya moyo (cardiac tests). Hii ni kwa ajili ya usalama wa wachezaji na
waamuzi.
4. Hadi leo chama cha Madaktari Tanzania, TASMA hakina ofisi. Hii ni aibu kwa chama chenye
hadhi na umuhimu wa kipekee kama hiki. Tutahakikisha TASMA inapata ofisi yake pamoja
na chumba maalum cha kliniki.
5. Huduma ya afya lazima iwe sehemu maalum ya mfumo wa idara ya ufundi. Ni muhimu timu
ya madaktari wa Timu ya Taifa (National Medical team) ijulikane ni kina nani na wapewe
mikataba ya kazi. Hii tutalipigania.
6. Majeraha ya michezo huwa yanahitaji utaalam wake wa tiba. Tutaiomba Serikali itupe
ushirikiano ili kipatikane kitengo maalum cha kutibu majeraha ya wanamichezo (sports
injuries wing) katika baadhi ya hospitali zetu wakati tunajiandaa kuwa na kitengo cha tiba
(Rehabilitation Centre) katika kituo cha michezo kitakachojengwa.
7. Ili kuimarisha uwezo wa madaktari wetu kutoa huduma za afya kwa wanamichezo,
tutahakikisha madaktari wengi kadiri iwezekanavyo wanapata kozi za msingi,kati na juu
(preliminary,intermediate and advanced). Nafasi hizi zitatolewa bila upendeleo wala kujuana.
8. Utoaji wa ushauri nasaha kwa wachezaji utaongezeka hasa kuhusu masuala ya ukimwi na
madhara ya madawa ya kuongeza nguvu na ya kulevya.
1.8 Waamuzi
Imepita miaka zaidi ya 15 toka Tanzania itoe mwamuzi wa kimataifa wa kuchezesha fainali kubwa
(mara ya mwisho AFCON 1998), hii si sawa. Utaratibu uliopo sasa wa kuwapata na kuwaendeleza
waamuzi ama una mapungufu au haufai kabisa hivyo budi utafutwe utaratibu ulio mzuri zaidi katika
kupata waamuzi bora, tafiti zitafanywa ili kubaini ni njia zipi za kisayansi za kuwapata waamuzi bora
(Top referees).Semina za mara kwa mara za CAF na FIFA ni nzuri lakini hazitoshi, TFF lazima
iwekeze kwa kutoa mafunzo zaidi ya waamuzi kwa gharama zake.
Aidha mradi wa maendeleo ya mpira kwa vijana (grassroot) utahusisha pia mafunzo ya uamuzi wa
mpira kwa vijana kama kinavyofanya kituo cha Jenerali Twalipo.
Utaratibu wa kutoa adhabu kwa waamuzi wanaosemekana wameboronga uwanjani nao unahitaji
marekebisho ya haraka sana. Uamuzi wa mpira ni taaluma kama zilivyo taaluma nyingine,mwamuzi
akikosea ni vyema akakosolewa na mwamuzi mwenzie ambaye ni mwandamizi,na kama ni
kuadhibiwa aadhibiwe na jopo la waamuzi wenzie waandamizi lakini wastaafu na sio mtu mwingine
ambaye hajawahi kupuliza filimbi.
1.9 Makocha
Kumekuweko na utamaduni usiofaa katika soka la Tanzania miaka ya karibuni wa kuona kuwa
makocha wa kigeni ndio bora zaidi na wanastahili mikataba,mishahara minono na marupurupu
ilhali makocha wazawa wanageuzwa ‘deiwaka’, jambo hili ni baya sana,ajira ziheshimiwe kwa
msingi wa taaluma na sio kwa msingi wa nchi atokayo mtu.
Makocha wetu wazalendo wana uwezo mkubwa kama wakipewa nyenzo kama wanazopatiwa
wageni, kama malipo mazuri, mikataba ya muda mrefu, vitendea kazi na kuheshimiwa program
zao bila kuingiliwa na viongozi.Iwapo nitachaguliwa ninaahidi:
- Kuwaendeleza makocha kimafunzo ndani na nje ya nchi kwa wale wenye uwezo na
utashi wa kufanya hivyo.
- Kushawishi taasisi za elimu nchini kama vyuo vikuu kufundisha taaluma ya ukocha
- Kuhakikisha walimu wa mpira wa timu zetu za Taifa wanakuwa na mikataba stahiki, hii
ni pamoja na benchi zima la ufundi.
- Kuwajengea uwezo makocha wetu wazalendo ili nao wapate fursa ya kufundisha mpira
nje ya nchi.
- Kuanzisha tuzo za kila mwaka za makocha wazalendo ambao wamefanya vizuri katika
ufundishaji wa soka la vijana la wanawake na wanaume.
- Kuhakikisha utaratibu wa leseni za CAF unazingatia vigezo vya kitaaluma, uzoefu na
ushiriki wa kocha mhusika katika ufundishaji. Makocha ambao wanafundisha (active
coaches) watapewa kipaumbele katika kupata kozi za kupanda madaraja kuliko wale
wanaofungia vyeti makabatini.Leseni za CAF ni muhimu katika kumfanya mwalimu wa
mpira atambulike kimataifa.
- Kuhakikisha kanuni za ligi zinasimamiwa vyema ikiwemo kanuni itakayomlazimisha
kila mwalimu wa ligi kuu na daraja la kwanza awe mwanachama wa TAFCA (chama
cha makocha nchini), walimu wa kigeni watapewa uanachama wa muda.
1.10 Timu za Taifa
Timu zetu za Taifa, ziwe za wakubwa au za vijana ndio kioo cha mpira wa Tanzania. Jitihada
zote lazima zifanyike kuhakikisha tunakuwa na timu nzuri za Taifa kuanzia za wakubwa
(wanawake/wanaume) hadi za vijana. Pamoja na jitihada zitakazofanyika kuboresha idara ya
ufundi kama ilivyoanishwa hapo juu lakini pia yafuatayo ni mambo ya ziada yatakayofanyika.
(a) Kuandaa fainali za Afrika za umri chini ya miaka 17 (U-17) mwaka 2019
Hadi sasa hakuna nchi ambayo imekwisha pata uenyeji wa mashindano haya. Uenyeji huu
unatolewa na Shirikisho la vyama vya mpira Afrika CAF.Hii ni changamoto kwetu
Watanzania kuomba uenyeji huu.Tukipewa fursa hii itatusaidia sana kutusukuma tuanze
kuandaa programu ya nguvu ya miaka mitano ya kupata timu yetu itakayocheza katika
fainali hizi kama wenyeji. Aidha kama nchi tutalazimika kuboresha miundo mbinu yetu
hususani viwanja vyetu vya mpira, jambo ambalo litatusaidia siku za usoni. Ninaamini
uwezo wa kuandaa mashindano haya kama nchi tunao. Nikichaguliwa nitalisimamia hili.
(b) Nidhamu
TFF itaandaa Kanuni za Nidhamu (code of ethics) kwa wachezaji, walimu na viongozi wa
Timu za Taifa mara wawapo ndani na nje ya uwanja. Hii itasaidia kujenga nidhamu ya
timu. Kanuni hizi zitaendana sambamba na kanuni za maadili za TFF.
(c) Walimu
Ni vyema siku za usoni timu zetu zote za Taifa zikafundishwa na makocha wazawa.
Utaratibu utafanyika kuhakikisha makocha wasaidizi ambao ni wazawa wanaendelezwa
kufikia kiwango hicho, hii itakuwa ni pamoja na kuwapatia fursa za mafunzo ndani na nje
ya nchi.
(d) Zanzibar
TFF kwa kushirikiana na Chama cha Mpira Zanzibar ZFA tutahakikisha kunakuwa na
mahusiano ya karibu ya walimu wa timu za Taifa Zanzibar na Bara ili kuhakikisha timu
bora ya Taifa inaundwa na vijana wa pande mbili za Muungano. Aidha jitahada za Zanzibar
kuwa mwanachama kamili wa CAF na FIFA zitaendelea kuungwa mkono.
2. Utawala
Inabidi tuendeleze utamaduni wa kuendesha shughuli za TFF kitaasisi (to have a corporate
culture).Nguzo muhimu za uendeshaji shirikisho kitaaluma ni pamoja na kujenga nidhamu ya
wafanyakazi,heshima kwa uongozi,utunzaji wa kumbukumbu,ukarimu kwa wageni,umakini
katika manunuzi na utunzaji wa fedha pamoja na kufanya kazi kwa malengo na kuhakikisha
malengo hayo yamefikiwa.
Maeneo yafuatayo yataboreshwa ili kuongeza ufanisi:
2.1 Ofisi za Mikoa na Vyama Shiriki
Kwa kuzingatia vyama vya Mikoa kuwa ndio muendelezo mkuu wa shughuli za TFF Mikoani,
ni muhimu ofisi za mikoa zikawa kielelezo cha ufanisi wa utendaji wa TFF. Ofisi za Mikoa
zitaboreshwa hasa kwa kupewa vitendea kazi hususani vifaa vya mawasiliano.
Vyama shiriki hadi sasa havina ofisi zenye hadhi ya vyama hivi, tutahakikisha tunaondoa aibu
hii. Aidha kutokana na mapato ya TFF sehemu ya mapato haya itatengwa kwa ajili ya ruzuku
ya kupeleka kwenye vyama vya Mikoa na vyama shiriki ili isaidie kupunguza makali ya
kuendesha vyama vyetu.
2.2 Ofisi ya Rais
Kutakuwa na ofisi ya Rais wa TFF. Ofisi ya Rais wa TFF (office of the President) lazima
iimarishwe na iwe sehemu itakayoweza kukabiliana na changamoto za maendeleo ya mpira
wa miguu. Rais wa TFF ndiye msimamizi mkuu wa shughuli za mpira wa nchi hii,lazima
awe na mahali stahili pa kufanyia kazi kulingana na hadhi yake.Hii itakuwa ni pamoja na
kuwa na wasaidizi wenye uweledi wa kutosha katika shughuli za kila siku za kuongoza
shirikisho.
Ofisi za TFF makao makuu uwanja wa Karume zitakarabatiwa na kuongeza nafasi ya
kufanyia kazi.
2.3 Maslahi
Maslahi ya wafanyakazi wa TFF yataboreshwa ili kuwaongezea motisha. Hii itakuwa ni
pamoja na kuwapa fursa ya kuhudhuria mafunzo mbalimbali.
2.4 Vilabu vya Mpira
Vilabu vitasaidiwa kupewa mwongozo wa kujiendesha kwa ufanisi zaidi. Aidha utaratibu wa
mgawanyo wa mapato ya milangoni utatazamwa upya kwa lengo la kuhakikisha vilabu
vinapata mgao mkubwa kuliko iliyo sasa. Hii ni kwa kuzingatia gharama kubwa wanazoingia
vilabu katika kuandaa timu ikiwemo malazi, usafiri, vifaa, posho, dawa, mishahara n.k.
2.5 Wachezaji wastaafu
Hii ni hazina ya Taifa,kustaafu kwao kucheza mpira sio mwisho wao wa kuchangia maendeleo
ya mpira wa nchi yetu.Jitihada zitafanyika kuanzisha mfuko maalum (Trust Fund) ambao
utachangiwa na wachezaji wenyewe wanapokuwa bado dimbani pamoja na TFF, hii ni kwa ajili
ya kuwasaidia hapo baadae wanapokuwa na matatizo hasa ya ugonjwa. Aidha chama cha
wachezaji wastaafu (SPUTANZA) kitapewa ofisi na kitaimarishwa ili kiwe kiungo muhimu
kati ya wachezaji na TFF.Wachezaji watahimizwa watumie chama hiki kutatua matatizo yao na
chama kitapewa fursa kikanuni ya kuwa mtetezi mkuu na msimamizi wa maslahi ya wachezaji.
2.6 Mikataba
Utaratibu wa TFF kuingia mikataba na wadhamini mbalimbali utarekebishwa ili kuongeza
uwazi. Ipo mikataba ambayo imesainiwa na TFF ambayo imesababisha vyama vya mikoa na
wilaya, pamoja na uhaba wao wa pesa, wahangaike kutafuta fedha za zaida kuandaa timu zao
kwa ajili ya mashindano yanayobeba jina la mdhamini kwa kuwa fedha anayotoa mdhamini
haikidhi uendeshaji wa mashindano yenyewe.
Aidha vipengele tata vinavyokandamiza maslahi ya vilabu katika baadhi ya mikataba
inayosainiwa kati ya TFF na wadhamini vitarekebishwa kama sio kuondolewa kabisa kwa
maslahi ya ustawi wa mpira wetu. Haki za vilabu katika matangazo ya biashara yahusuyo
mpira zitalindwa kwa nguvu zote.
2.7 Utaratibu wa Mashindano
Yapo mashindano ya vijana kama Umiseta na Umitashumta yanayoandaliwa na Serikali. Kuna
wakati mashindano kama haya yanafanyika sambamba na mashindano yanayoandaliwa na TFF
kama vile Copa Coca Cola. Yote haya ni mashindano ya vijana, na washiriki wanakuwa ni
vijana toka shule hizo hizo. Kwa nini tugombee fito wakati tunajenga nyumba moja? Ni
vyema kalenda ya mashindano ya vijana kitaifa ikaandaliwa kwa pamoja kati ya Serikali na
TFF.
2.8 Usajili wa Vyama vya Mpira vya Wanawake
Usajili huu haujakamilika nchini nzima hususani ngazi ya wilaya. Juhudi zitafanyika
kukamilisha zoezi hili ili mpira wa wanawake uenee kote Tanzania.
2.9 Kitengo cha habari
Kitengo hiki kitaboreshwa kwa kuongezewa nyenzo za kufanyia kazi na kukipatia fursa zaidi
za mafunzo. Aidha majukumu yake yataongezwa ili pia kishughulikie mahusiano ya
kimataifa.Hivyo kama nikichaguliwa nitapendekeza mkuu wake aitwe ‘Afisa habari na
mahusiano ya kimataifa’.
3. Masoko na Uwekezaji
Mpira unaendeshwa kwa fedha nyingi. TFF ili iweze kujiendesha kwa ufanisi ni lazima iwe na
vyanzo vya uhakikika vya mapato. Ili kufanikisha azma hii kitengo cha masoko na uwekezaji
kitahakikisha kwamba:
1. TFF inatengeneza utaratibu mzuri wa kuuza bidhaa zake ndani na nje ya nchi kwa kupitia
uuzaji wa kawaida na wa mtandao.Mikataba itaandaliwa ili kudhibiti uuzwaji holela wa
bidhaa za TFF.
2. Vyumba vya Maduka vinajengwa kuzunguka uwanja wa Karume na kukodishwa.
3. Jengo la kitega cha uchumi litajengwa kwenye ardhi ya Uwanja wa Karume.Pia jukwaa la
watazamaji litajengwa uwanja wa Karume ili mechi ambazo sio kubwa ziweze kufanyika
pale, hii itaviongezea vilabu mapato.
4. Juhudi za kuboresha ukusanyaji, usimamizi na mgawanyo wa haki wa mapato ya milangoni
yatokanayo na ligi yetu utaboreshwa ikiwa ni pamoja na kubuni vyanzo vipya kupitia njia
mbali mbali zikiwemo za udhamini mbadala kwa vilabu.Aidha jitihada ambazo tayari
zimekwisha anza za kuunda bodi ya kuendesha ligi na uanzishwaji wa utaratibu huru wa
kuendesha ligi zitaendelezwa ili kuongeza ufanisi,kuinua mapato ya vilabu na kuongeza
msisimko wa ligi.Ninaunga mkono juhudi hizi.
5. Viwanja vingi vya mpira nchini vinamilikiwa aidha na Halmashauri,Serikali kuu
au vyama vya siasa.Viwanja hivi vingi viko katika hali mbaya kuanzia nyasi ,hali
ya uzio,vyumba vya kubadilishia nguo,mageti,vifaa vya kuzimia moto n.k.ni
vyema TFF na vyama vya mikoa kwa kupitia utaratibu wa PPP (Public Private
Sector Partnership) vikaingia ubia na wamiliki wa viwanja hivi ili TFF na
washirika wake wachukue jukumu la kuviboresha,kuvisimamia na kuviendesha ili
kuhakikisha vinakuwa katika viwango stahili kwa mujibu wa kanuni za FIFA na
CAF.Hii itaongeza usalama wa wachezaji na watazamaji na kuinua mapato
yatokanayo na viwanja hivi
Ushiriki wa wadau
Kwa sasa taswira ya mpira wa miguu inawafungia nje wadau wengi ambao kama wangepewa fursa
ya kushiriki nao wangetaka wachangie maendeleo ya mpira wa miguu.Juhudi kubwa inabidi zitumike
kurudisha imani hii ili kuleta hisia za umoja wa kitaifa katika kuendesha mpira wetu (sense of
belongingness) .Ni muhimu taasisi muhimu za kitaifa zishirikishwe katika sekta hii ya mpira wa
miguu ,hii ni pamoja na taasisi kama Tacaids,Mashirika ya utalii kama TANAPA na TTB,Umoja wa
wafanyabiashara kama TPSF,CTI na TCCIA ,Kituo cha uwekezaji TIC n.k.Ushirikiano huu utasaidia
kujenga jina la Tanzania pale tunapoandaa michuano ya kimataifa na pia kuhamasisha vijana wetu
waepuke maisha hatarishi kama vile kujihusisha na ngono isiyokuwa salama,madawa ya kulewa
(kutumia na kusafirisha),ulevi wa kupindukia n.k.
HITIMISHO
Ndugu zangu,nihitimishe kwa kusisitiza kuwa maendeleo ya mpira Tanzania kwa hapa
yalipofikia yanahitaji ubunifu,ujasiri na msukumo mpya ili tuweze kuunyanyua mpira wetu na
kuupa mwelekeo mpya,mwelekeo wa matumaini ,mwelekeo wa kulipeleka soka letu katika
kushinda vikombe vikubwa barani mwetu Afrika na Duniani.
Shime wapiga kura nipeni fursa hii ya kuwa Rais wa TFF ili kwa pamoja tukishirikiana na
wadau wote muhimu katika sekta yetu tuweze kulisikuma gurudumu hili ili hatimae soka iweze
kuiletea nchi yetu sifa na kuwapa raha mamilioni ya watanzania wapenda mpira.
Pamoja tutaweza
Chagua MALINZI
Chagua MABADILIKO
Mungu ibariki Afrika
Mungu ibariki Tanzania
Jamal Malinzi
Mgombea nafasi ya Urais
TFF
2013
Mpira ni afya, mpira ni burudani, mpira ni ajira kwa vijana!
MAELEZO BINAFSI YA JAMAL EMIL MALINZI MGOMBEA URAIS TFF
Tarehe ya kuzaliwa : 08 Agosti, 1960
Elimu: 1974-1977 : Sekondari O-Level
Mwanza Secondary School
1978-1981 : A-Level
Ilboru High School
1980-1981 : JKT – Ruvu
Operesheni TIJA
1981-1985 : Chuo Kikuu Dar Es Salaam
Digrii ya Uhandisi (Upper 2nd Class)
1986-1993 : Ajira -Coopers and Lybrand
Tanzania Industrial Research
and Development Organization
1993-Hadi Leo : Mjasiriamali
Mkurugenzi – Cargostars Limited
Michezo : Nimekuwa promota wa mchezo wa ngumi za kulipwa
kuanzia kipindi cha 1995-2001. Baadhi ya mabondia
wangu walifikia kiwango cha kimataifa hadi kusaini
mkataba na Promota maarufu duniani Don King.
: Nimekuwa Seneta wa Yanga na baadae nikawa
Mkurugenzi na mwisho nikawa Katibu Mkuu wa Klabu
ya Yanga kati ya mwaka 1999 na 2005.
: Nimekuwa Mkurugenzi na Msimamizi Mkuu wa Timu ya
Mkoa wa Dar Es Salaam ya Mzizima United. Timu hii
ndiyo ya mwisho kushinda Kombe la Taifa mwaka 2007
ikiwa timu moja ya Mkoa wa Dar Es Salaam.
: Nimekuwa mjumbe wa Baraza la michezo la mkoa wa
Dar es salaam 2009-2011
: Nimekuwa Mwenyekiti wa kamati ya mashindano mkoa
wa Pwani 2009-2011
: Hadi sasa mimi ni mwenyekiti wa Chama cha mpira wa
miguu mkoa wa Kagera
: Kikampuni, Kampuni yetu ya Cargostars Limited ina
uzoefu wa muda mrefu wa kudhamini michezo
mbalimbali. Kwa kipindi cha miaka saba Cargostars
Limited iliidhamini mbio za marathon za wabunge.
Aidha Cargostars Limited ina rekodi ya kudhamini
michezo mingine kadhaa ikiwemo mpira wa miguu,
ngumi, Tennis na Golf.

22 October 2013

MAREFA SIMBA, YANGA WALA MILIONI MOJA



Makamu wa Pili wa Rais wa Shirikisho la Mpira wa Miguu Tanzania (TFF), Ramadhan Nassib ametoa sh. milioni moja kwa waamuzi waliochezesha mechi ya Simba na Yanga iliyochezwa wikiendi iliyopita jijini Dar es Salaam.

Nassib ambaye alichaguliwa katika nafasi hiyo akiwakilisha klabu amesema ametoa fedha hizo ili kuwapongeza waamuzi hao kwa kuchezesha vizuri mechi hiyo iliyomalizika kwa sare ya mabao 3-3.

“Waamuzi wanapofanya vibaya tunawaadhibu, hivyo wakifanya vizuri wanastahili kupongezwa pia. Vilevile kuwapongeza ni kuwaongezea ari ya kuchezesha vizuri zaidi,” amesema.

Israel Nkongo ndiye aliyeongoza jopo hilo ambapo mwamuzi msaidizi namba moja alikuwa Hamis Chang’walu wakati namba mbili alikuwa Ferdinand Chacha. Mwamuzi wa mezani alikuwa Oden Mbaga.


Waamuzi wote hao wana beji za Shirikisho la Kimataifa la Mpira wa Miguu (FIFA), na watoka Dar es Salaam ukiondoa Chacha ambaye maskani yake ni Bukoba mkoani Kagera.

SERENGETI BOYS YAALIKWA MICHUANO YA ANOCA


Timu ya Taifa ya Tanzania kwa vijana wenye umri chini ya miaka 20 (Serengeti Boys) imealikwa kushiriki Olimpiki ya Afrika itakayofanyika Mei mwakani.

Mpira wa miguu ni kati ya michezo 22 itakayoshindaniwa katika mashindano yatakayofanyika Gaborone, Botswana chini ya Kamati za Olimpiki za Afrika (ANOCA).

Kwa mujibu wa Kamati ya Olimpiki ya Tanzania (TOC), Tanzania imepewa nafasi ya kushiriki katika michezo hiyo ya Olimpiki kwa Afrika kutokana na kuwa na programu nzuri za vijana hasa chini ya umri wa miaka 17.

Hiyo itakuwa ni michezo ya Pili ya Afrika kwa Olimpiki ambapo ya Kwanza ilifanyika mwaka 2010 jijini Rabat, Morocco.

21 October 2013

MIL 500 NDIZO ZILIZOPATIKANA JANA






Mechi ya Ligi Kuu ya Vodacom (VPL) ya watani wa jadi Simba na Yanga iliyochezwa jana (Oktoba 20 mwaka huu) kwenye Uwanja wa Taifa, Dar es Salaam na kumalizika kwa sare ya mabao 3-3 imeingiza sh. 500,727,000.

Washabiki 57,422 ndiyo waliokata tiketi kushuhudia pambano hilo namba 63 kwa viingilio vya sh. 5,000, sh. 7,000, sh. 10,000, sh. 15,000, sh. 20,000 na sh. 30,000.

Ni tiketi 131 tu ndizo hazikuuzwa ambazo ni 90 za VIP A, 40 za VIP B na moja ya VIP C. Tiketi zilizochapwa kwa ajili ya mechi hiyo ni 57,558 ambayo ndiyo idadi ya viti vilivyopo kwenye uwanja huo.

Kila klabu imepata mgawo wa sh. 123,025,564.32 wakati Kodi ya Ongezeko la Thamani (VAT) iliyolipwa ni sh. 76,382,084.75.

Mgawo mwingine wa mapato hayo ni asilimia 15 ya uwanja sh. 62,555,371.69, tiketi sh. 7,309,104, gharama za mechi sh. 37,533,223.01, Kamati ya Ligi sh. 37,533,223.01, Mfuko wa Maendeleo ya Mpira wa Miguu (FDF) sh. 18,766,611.51 na Chama cha Mpira wa Miguu Mkoa wa Dar es Salaam (DRFA) sh. 14,596,253.39.

WANAWAKE WABADILI RATIBA VPL





Kamati ya Ligi ya Shirikisho la Mpira wa Miguu Tanzania (TFF) imefanya marekebisho ya ratiba ya Ligi Kuu ya Vodacom (VPL) ili kupisha mechi ya mchujo ya Kombe la Dunia kati ya Tanzania na Msumbiji.

Mechi hiyo ya kwanza ya raundi ya kwanza kwa mashindano ya wanawake wenye umri chini ya miaka 20 itachezwa Jumamosi (Oktoba 26 mwaka huu) Uwanja wa Taifa, Dar es Salaam kuanzia saa 10 jioni.
U20 tayari imehamishia kambi yake hosteli ya Msimbazi Center, Dar es Salaam kutoka JKT Ruvu mkoani Pwani tangu wiki iliyopita kujiandaa kwa mechi hiyo. Fainali za Kombe la Dunia kwa U20 wanawake zitafanyika mwakani nchini Canada.

Marekebisho ya ratiba ya VPL yamegusa raundi zote tatu zilizobaki kukamilisha mzunguko wa kwanza. Kutokana na marekebisho hayo mechi za raundi ya 11 zitakuwa ifuatavyo; Oktoba 28 mwaka huu ni Coastal Union vs Mtibwa Sugar, Oljoro JKT vs Ashanti United, Ruvu Shooting vs Kagera Sugar na Simba vs Azam. Oktoba 29 mwaka huu ni Tanzania Prisons vs Mbeya City, Yanga vs Mgambo Shooting na Rhino Rangers vs JKT Ruvu.

Raundi ya 12 ni kama ifuatavyo; Oktoba 31 mwaka huu ni Simba vs Kagera Sugar, Novemba 1 mwaka huu ni JKT Ruvu vs Yanga. Novemba 2 mwaka huu ni Mgambo Shooting vs Coastal Union, Tanzania Prisons vs Oljoro JKT, Azam vs Ruvu Shooting, Mtibwa Sugar vs Rhino Rangers na Mbeya City vs Ashanti United.

Raundi ya 13 ni kama ifuatavyo; Novemba 6 mwaka huu ni JKT Ruvu vs Coastal Union, Ashanti United vs Simba, Kagera Sugar vs Mgambo Shooting, Rhino Rangers vs Tanzania Prisons na Ruvu Shooting vs Mtibwa Sugar. Novemba 7 mwaka huu ni Azam vs Mbeya City.

Mechi za kufunga raundi ya 10 zitachezwa keshokutwa (Oktoba 23 mwaka huu) kama ratiba inayoonesha. Mechi hizo ni kati ya Coastal Union vs Simba, Tanzania Prisons vs Kagera Sugar na Yanga vs Rhino Rangers.

18 October 2013

MBWEZELENI ATAJA WANAOTAKIWA KUGOMBEA KAMATI YA LIGI.



Kamati ya Uchaguzi ya Shirikisho la Mpira wa Miguu Tanzania (TFF) imetangaza orodha ya mwisho ya wagombea wa uchaguzi wa TFF na wa Bodi ya Ligi (TPL Board) utakaofanyika baadaye mwezi huu.


Uchaguzi wa Bodi ya TPL utafanyika Oktoba 25 mwaka huu wakati ule wa TFF utafanyika Oktoba 27 mwaka huu. Kampeni kwa ajili ya uchaguzi wa TPL Board na ule wa TFF zimeanza leo (Oktoba 18 mwaka huu) zitamalizika siku moja kabla ya uchaguzi saa 10 kamili alasiri.

Mwenyekiti wa Kamati ya Uchaguzi, Hamidu Mbwezeleni amewataja wagombea kwa upande wa TPL Board kugombea uenyekiti ni Hamad Yahya Juma (Mtibwa Sugar), Makamu Mwenyekiti ni Said Muhammad Said Abeid (Azam). Wanaowania ujumbe wa Bodi ya Uendeshaji ni Kazimoto Miraji Muzo (Pamba) na Omary Khatibu Mwindadi (Mwadui).

Wagombea kwenye uchaguzi wa TFF ni Athuman Jumanne Nyamlani na Jamal Emily Malinzi (Rais), Imani Omari Madega, Ramadhan Omar Nassib na Wallace Karia (Makamu wa Rais).

Kwa upande wa wajumbe wa Kamati ya Utendaji ni Kalilo Samson (Kanda namba 1- Geita na Kagera), Jumbe Odessa Magati, Mugisha Galibona, Samwel Nyalla na Vedastus Lufano (Kanda namba 2- Mara na Mwanza), Epaphra Swai na Mbasha Matutu (Kanda namba 3- Shinyanga na Simiyu).

Ali Mtumwa, Elley Simon Mbise na Omar Walii Ali (Kanda namba 4- Arusha na Manyara), Ahmed Idd Mgoyi na Yusuf Hamis Kitumbo (Kanda namba 5- Kigoma na Tabora), Ayubu Nyaulingo na Blassy Mghube Kiondo (Kanda namba 6- Katavi na Rukwa), Ayoub Shaibu Nyenzi, David Samson Lugenge, John Exavery Kiteve, Lusekelo Elias Mwanjala (Kanda namba 7- Iringa na Mbeya).

James Patrick Mhagama na Stanley William Lugenge (Kanda namba 8- Njombe na Ruvuma), Athuman Kingombe Kambi, Francis Kumba Ndulane na Zafarani Mzee Damoder (Kanda namba 9- Lindi na Mtwara), Hussein Zuberi Mwamba, Stewart Ernest Masima, Charles Komba (Kanda namba 10- Dodoma na Singida), Farid Nahdi, Geofrey Irick Nyange, Juma Abbas Pinto, Riziki Juma Majala) na Twahil Twaha Njoki (Kanda namba 11- Morogoro na Pwani).

Davis Elisa Mosha, Khalid Abdallah Mohamed (Kanda namba 12- Kilimanjaro na Pwani), Alex Crispine Kamuzelya, Kidao Wilfred Mzigama, Muhsin Said Balhabou na Omary Isack Abdulkadir (Kanda namba 13- Dar es Salaam).

Mbwezeleni amewataka wagombea kufanya kampeni bila kukashfu wenzao, kwani Kanuni ya Uchaguzi za TFF toleo la 2013 inatoa fursa kwa Kamati ya Uchaguzi kuwaondoa wagombea wa aina hiyo kwenye uchaguzi.




17 October 2013

SHAFI DAUDA ANASEMA NI ZENGWE TU TFF ALIPA FAINI TFF (SIKIZA SAUTI)






Baada ya Kamati Maadili kubaini kuwa Shaffih Dauda,  mwanafamilia wa TFF katika taarifa iliyotumwa kutoka katika shirikisho hilo  na kugungundua kuwa ni Mwenyekiti wa Bombom FC, kwani fomu yake ya kuomba uongozi ilipitishwa na klabu ya Simba na pia ameshakuwa kiongozi katika ngazi mbalimbali ndani ya Chama cha Mpira wa Miguu Wilaya ya Kinondoni (KIFA), hivyo yeye ni ‘Mwanafamilia  waTff  kwa mujibu wa kifungu cha 2(v) cha Kanuni za Utii za TFF toleo la 2013.




Na kumpa  onyo kali na faini ya sh. milioni moja anayotakiwa kuilipa ndani ya siku tatu Nimemyafuta shafii dauda kwa njia ya simu





Akilipa faini ataweza kuendelea na mchakato wa kugombea nafasi ya uongozi aliyoomba.

BOFYA  HAPA USIKIZE



15 October 2013

UKATA WAIONDOA MALAWI KOMBE LA CHALENJI



Baraza la vyama vya soka Afrika mashariki na kati limepata pigo baada ya timu mwalikwa maarufu kama mware wa Nyasa ,Malawi kujitoa katika michuano hiyo ya Chalenji baada ya kukosa fedha za kuendesha timu hizo .

Jambo hili linakuja baada ya Nchi hiyo kusimamisha shughuri zote za kimaendeleo ya soka kwa timu za vijana na wakubwa kwa ukosefu wa pesa.

Michuano hiyo inayotarajiwa kuanza Nov 27 na kumalizika Dec 12 nchini Kenya .

Mapema wiki hii ,Katibu mkuu wa Cecafa Nicholas Musonye ametangaza kuwa Cote d’Ivoire haitashiriki michuano kutokana na matatizo ya kiuchumi

Kwa maana hiyo timu ya vijana ya malawi chini ya miaka 20 haitashiriki michuano hiyo itakayofanyika Lesotho mwishoni mwa mwaka huu .

Rais wa Chama soka cha malawi  Walter Nyamilandu, ambaye alinukuliwa na chombo cha cha habari cha nchi hiyo ,Hwajapokea mwaliko kutoka Cecaafa na hata wakipokea hawatoshiriki kwani hawana pesa  .

Ujumbe wa Hija wa Walii Amri wa Waislamu wa Mwaka 1434 Hijria


Kwa jina la Allah Mwingi wa rehema Mwenye Kurehemu
Na hamdu na sifa zote njema ni za Mwenyezi Mungu Mola Mlezi wa viumbe vyote, na rehma na amani zimshukie Bwana wa Manabii na Mitume na Aali zake watukufu na masahaba zake wema.
Kuwadia kwa msimu wa Hija kunapasa kuhesabiwa kuwa ni Idi kubwa kwa umma wa Kiislamu. Ni fursa adhimu wanayopata Waislamu duniani katika masiku haya yenye thamani kubwa, na ni tiba ya kimiujiza ambayo kama itajulikana thamani yake na kama itatumiwa kama inavyostahiki, itakuwa dawa ya kuondoa madhara mengi yaliyousibu na yanayoweza kuusibu Ulimwengu wa Kiislamu.
Hija ni chemchemi ya rehma za Mwenyezi Mungu. Kila mmoja wenu nyinyi mahujaji mliopata saada, mnayo bahati hii kubwa ya kuzitumia amali hizi zilizojaa usafi na umaanawi kwa ajili ya kuzikosha nyoyo na roho zenu, na kuchukua kwenye hazina hii ya rehma, izza na nguvu akiba kwa ajili ya umri wenu wote uliobakia. Khushuu na unyenyekevu mnaouonyesha mbele ya Mwenyezi Mungu Mola Mrehemevu; ahadi mnayochukua ya kutekeleza majukumu waliyopewa Waislamu; uchangamko, harakati na uchukuaji hatua za kutekeleza mambo ya dini na dunia; kuwa na huruma na usamehevu katika kuamiliana na ndugu zenu; kuwa na ujasiri na moyo wa kujiamini katika kuyakabili matukio mazito; kuwa na matumaini ya kupata msaada na usaidizi wa Mwenyezi Mungu kila mahala na katika kila jambo; na kwa maneno mafupi ni kwamba mnaweza kuutumia uwanja huu wa mafunzo na malezi ya kidini wa kumwandaa Muislamu kwa ajili yenu wenyewe ili kuzipamba nafsi zenu kwa vito hivi na pia kuchukua kutoka kwenye hazina hizo zawadi kwa ajili ya nchi zenu, mataifa yenu na umma mzima wa Kiislamu.
Leo umma wa Kiislamu unahitajia kuliko kitu chochote kile kuwa na watu wanaoambatanisha fikra na matendo pamoja na imani, upendo na ikhlasi; na muqawama mbele ya maadui wenye kisasi sambamba na kuzijenga nafsi zao kimaanawi na kiroho. Hii ndio njia pekee ya kuiokoa jamii adhimu ya Waislamu na mazonge mbalimbali ya muda mrefu ambayo ama yanajulikana wazi kuwa yamesababishwa na adui au yametokana na udhaifu wa azma, imani na umaizi.
Hapana shaka kuwa zama hizi ni zama za mwamko na kurejea Waislamu kwenye utambulisho wao; uhakika huu unaweza kuonekana kwa uwazi kabisa kutokana na changamoto mbalimbali ambazo nchi za Waislamu zimekabiliana nazo. Na ni katika mazingira haya ambapo azma na irada inayotegemea imani, kutawakali, umaizi na tadbiri vinaweza kuyaletea ushindi na heshima mataifa ya Waislamu, na kuufanya mustakabali wao kuwa wenye izza na utukufu. Kambi wanayokabiliana nayo, ambayo haiwezi kuuvumilia mwamko na izza ya Waislamu imejitosa uwanjani kwa nguvu zake zote, na kutumia nyenzo zote za kiusalama, za kisaikolojia, za kijeshi, za kiuchumi na za kipropaganda kwa lengo la kuwavunja nguvu na kuwakandamiza Waislamu na kuwashughulisha wao kwa wao. Ukweli wa mengi unadhihirika kwa kutupia jicho hali ya nchi za Magharibi mwa Asia kuanzia Pakistan na Afghanistan hadi Syria, Iraq na Palestina, nchi za Ghuba ya Uajemi na vilevile nchi za kaskazini mwa Afrika kuanzia Libya, Misri na Tunisia hadi Sudan na nchi nyenginezo. Vita vya ndani, taasubi pogo za kidini na kimadhehebu; kukosekana uthabiti wa kisiasa; kuenea ugaidi wa kikatili; kujitokeza makundi na harakati zenye kufurutu mpaka za watu wanaovipasua vifua vya watu kwa namna zilivyokuwa zikifanya kaumu za kishenzi katika historia kisha kuutafuna kinyama moyo wa mtu; wanaobeba silaha na kuua watoto na wanawake; wanaowakata vichwa wanaume na kuwanajisi maharimu zao, na hata baadhi ya wakati wakatenda jinai hizi za kuaibisha na zenye kuchukiza kwa kutumia jina na bendera ya dini, yote hayo ni matokeo ya mpango wa kishetani na wa kiistikbari wa mashirika ya kiintelijinsia ya madola ya kigeni na maajenti wa tawala vibaraka yanazoshirikiana nazo katika eneo, na ambayo yanawezekana kujiri kutokana na mazingira yaliyoko ndani ya nchi mbalimbali na kuwaletea masaibu machungu wananchi wa mataifa hayo. Ni hakika kwamba katika hali na mazingira kama haya haiwezekani kutarajia kuwa nchi za Waislamu zitaweza kufanya marekebisho kwa kujaza fursa tupu za kimaada na kimaanawi na kupata amani, ustawi na maendeleo ya kielimu na uwezo imara kimataifa ambavyo ni matunda ya baraka za mwamko na kurejea kwenye utambulisho wao. Hali hizi za kuhuzunisha zinaweza kuviza Mwamko wa Kiislamu na kuupoteza utayarifu wa kiroho uliopatikana katika Ulimwengu wa Kiislamu; na kwa mara nyengine tena kuyaweka mataifa ya Waislamu katika hali ya kuzorota, kutengwa na kuporomoka kwa miaka mingine mingi, na kuyasahau masuala yao ya msingi na muhimu kama kuiokoa Palestina na kuyaokoa mataifa ya Waislamu na unyang'anyi wa Marekani na Uzayuni.
Dawa mujarabu na ya msingi inaweza kupatikana katika ibara mbili muhimu ambazo zote ni miongoni mwa mafunzo ya wazi kabisa ya Hija:
Mosi: Umoja na udugu wa Waislamu chini ya bendera ya tauhidi.
Pili: Kumtambua adui na kukabiliana na njama na mbinu zake.
Kuimarisha moyo wa udugu na mshikamano ni funzo kubwa la Hija. Katika mahala hapo ni marufuku hata kubishana na kuwatolea maneno watu wengine. Kuvaa vazi la aina moja, kufanya amali za namna moja na harakati za aina moja, na kuwa na tabia ya huruma katika mahala hapo kunamaanisha usawa na udugu wa watu wote wenye imani na wenye kufungamana na mhimili wa tauhidi. Hili ni jibu la wazi kabisa la Uislamu kwa kila fikra, itikadi na wito unaolitoa nje ya Uislamu kundi mojawapo la Waislamu wenye imani na Ala Kaaba na tauhidi. Watu wakufurishaji, ambao leo hii wamekuwa vikaragosi wa kutekeleza siasa za Wazayuni mahaini na waungaji mkono wao wa Magharibi, na ambao wanatenda jinai kubwa na kumwaga damu za Waislamu wasio na hatia; pamoja na wale wanaojidai kuwa Waswalihina na wale wanaojivika vazi la ushekhe, ambao wanakoleza moto wa hitilafu baina ya Shia na Suni na mfano wa hayo, wajue kwamba amali yenyewe ya Hija inayabatilisha madai yao. La kustaajabisha; wale watu ambao mkusanyiko wa kujibari na washirikina ambao asili yake inatokana na amali ya Mtume Mtukufu SAW wanauchukulia kuwa ni katika mabishano yaliyokatazwa, wao wenyewe wako mstari wa mbele katika kuchochea mizozano ya umwagaji damu kati ya Waislamu.
Mimi, kama walivyo maulama wengine wa Uislamu na wenye uchungu na umma wa Kiislamu, kwa mara nyengine tena ninatangaza kuwa, kauli yoyote na kitendo chochote kitakachosababisha kuwashwa moto wa hitilafu baina ya Waislamu, na vilevile kuyatusi matukufu ya lolote lile kati ya makundi ya Waislamu, au kuikufurisha mojawapo kati ya madhehebu za Kiislamu, ni kuitumikia kambi ya ukafiri na shirki na ni usaliti kwa Uislamu na ni haramu kidini.
Kumtambua adui pamoja na mbinu zake ndio nguzo ya pili. Kwanza kabisa haifai kughafilika na kusahau kwamba kuna adui mwenye kisasi; na amali ya mara kadhaa ya kumrembea mawe Shetani huko Jamarati katika Hija ni alama ya mfano wa kulikumbuka jambo hilo akilini muda wote. Pili, haitakiwi kufanya makosa katika kumtambua adui wa asili, ambaye leo hii ni hiyo kambi ya Uistikbari wa dunia na mtandao mtenda jinai wa Uzayuni; na tatu, inapasa kuzielewa vizuri mbinu zinazotumiwa na adui huyu mwenye inadi, ambazo ni kuchochea mifarakano baina ya Waislamu, kueneza ufisadi wa kisiasa na kiakhlaqi, kuwatisha na kuwarubuni wenye vipawa, kutoa mashinikizo ya kiuchumi kwa mataifa, na kueneza shaka katika imani za Kiislamu; na vilevile kuwatambua vibaraka na wasaidizi wao, ambao kwa kujua au kwa kutojua, wanawasaidia katika njia.
Madola ya Kiistikbari, na la mbele kabisa Marekani, yanatumia msaada wa nyenzo za vyombo vingi na vya kisasa vya habari ili kuficha sura yao halisi; na huku yakijidai kuwa waungaji mkono wa haki za binadamu na demokrasia huonyesha muamala wa kutaka kuzihadaa fikra za waliowengi katika mataifa. Huwa yanadai kutetea haki za mataifa katika hali ambayo, zaidi ya ilivyokuwa huko nyuma, mataifa ya Waislamu yanauhimili kila siku kwa mwili na roho zao moto wa fitina unaowashwa na madola hayo. Kwa kulitupia jicho taifa madhulumu la Palestina ambalo kwa miaka na miaka linaenedelea kupata majeraha ya jinai za utawala wa Kizayuni na waungaji mkono wake; au nchi za Afghanistan, Pakistan na Iraq ambazo maisha ya wananchi wao yamekuwa machungu kutokana na ugaidi ulioletwa na siasa za Uistikbari na wasaidizi wake wa eneo, au nchi ya Syria, ambayo kwa kosa la kuunga mkono harakati ya muqawama dhidi ya Uzayuni inaandamwa na wimbi la uadui la mabeberu wa kimataifa na watendaji wao wa eneo na kutumbukizwa kwenye vita vya ndani vya umwagaji damu, au nchi za Bahrain au Myanmar, ambazo kila moja kwa namna yake, Waislamu wanaoteseka wamesahauliwa, na maadui zao wanasaidiwa na kuungwa mkono, au kwa kuyaangalia mataifa mengine ambayo yanaandamwa na mashambulio mtawalia ya kijeshi, au vikwazo vya kiuchumi au hujuma za kiusalama, yote hayo yanaweza kuwadhihirishia watu wote sura halisi ya viranja hao wa mfumo wa ubeberu.
Wenye vipawa vya kisiasa, vya kiutamaduni na vya kidini wa kila mahala katika Ulimwengu wa Kiislamu wajijue kwamba wana wajibu wa kuufichua ukweli huu. Hili ni jukumu letu sote la kiakhlaqi na kidini. Nchi za kaskazini mwa Afrika, ambazo kwa masikitiko leo hii zimekumbwa na hitilafu kubwa za ndani zinapaswa kulizingatia zaidi jukumu hili adhimu, yaani kumtambua adui, mbinu na hila zake. Kuendelea hitilafu baina ya mirengo ya kitaifa na kughafilika na hatari ya vita vya ndani katika nchi hizi ni hatari kubwa ambayo hasara yake kwa umma wa Kiislamu haitoweza kufidika haraka.
Sisi, bila ya shaka hatuna shaka kwamba wananchi wa mataifa ya eneo waliosimama kidete wakautekeleza kivitendo Mwamko wa Kiislamu, kwa idhini ya Mwenyezi Mungu hawatoruhusu alama za nyakati zirudi nyuma na kurejea tena zama za watawala waovu, vibaraka na madikteta; lakini kughafilika na nafasi ya madola ya Kiistikbari katika kuzusha fitina na uingiliaji wao wa uharibifu kutaifanya kazi yao iwe ngumu na kuzirudisha nyuma kwa miaka na miaka zama za izza, amani na ustawi. Sisi tuna imani ya dhati ndani ya nyoyo zetu juu ya uwezo wa mataifa na nguvu ambazo Mwenyezi Mungu Mwenye hekima ameupa umma wa wananchi katika azma, imani na umaizi; na hilo tumejionea kwa macho yetu na kupata tajiriba kwa nafsi zetu kwa zaidi ya miongo mitatu katika Jamhuri ya Kiislamu ya Iran; tunachojitahidi kufanya ni kutoa wito kwa mataifa yote ya Waislamu wa kuifuata tajiriba hii ya ndugu zao katika nchi hii yenye heshima na isiyochoka.
Ninamwomba Mwenyezi Mungu Mtukufu yale yenye maslaha kwa Waislamu na kuwakinga na vitimbi vya maadui. Na ninamwomba akutakabalieni Hija yenu nyinyi nyote mahujaji wa Nyumba ya Mwenyezi Mungu, na akupeni uzima wa kimwili na kiroho na atiya ya akiba kubwa ya kimaanawi.
Wassalamu Alaykum Warahmatullahi Wabarakatuh
Sayyid Ali Khamenei
Tarehe 5 Dhilhijjah 1434 inayosadifiana na tarehe 19 Mehr 1392

11 October 2013

NYALLA, NYAULINGO, NYENZI HAWANA HATIA



Kamati ya Rufani ya Uchaguzi ya Shirikisho la Mpira wa Miguu Tanzania (TFF) imewarejesha warufani wote watatu katika kinyang’anyiro cha uchaguzi wa Kamati mpya ya Utendaji ya TFF utakaofanyika Oktoba 27 mwaka huu jijini Dar es Salaam.

Samwel Nyalla, Ayubu Nyaulingo na Ayoub Nyenzi walikata rufani mbele ya Kamati hiyo inayoongozwa na Jaji wa Mahakama ya Rufani Tanzania, Bernard Luanda kupinga uamuzi wa Kamati ya Uchaguzi ya TFF kuwaondoa katika uchaguzi huo ambapo wote wanagombea ujumbe wa Kamati ya Utendaji kuwakilisha kanda mbalimbali.

Akisoma uamuzi wao leo (Oktoba 11 mwaka huu) mbele ya Waandishi wa Habari kwenye ofisi za TFF, Jaji Luanda amesema baada ya kusikiliza hoja za Mrufani Nyalla walipitia Kanuni za Uchaguzi za TFF na kugundua yafuatayo;

Ibara ya 10(3) imeweka masharti makuu mawili ya ujazaji wa fomu za kugombea uongozi. Fomu hiyo ni lazima iwe na saini ya mgombea na ni lazima ithibitishwe na viongozi wa shirikisho.
Kamati imepitia Kanuni za Uchaguzi haijaona sehemu fomu hiyo ya uongozi imeambatanishwa ili kuifanya kuwa Kanuni ya Uchaguzi. Ni maoni ya Kamati kuwa ni vizuri fomu za kugombea zikawa ni sehemu ya Kanuni za Uchaguzi.

Kwa vile Kanuni za Uchaguzi za TFF za 2013 pia hazijaainisha nini adhabu kwa mgombea aliyekosea kujaza Fomu namba 1 ya kugombea uongozi, Kamati inaona itakuwa si haki kumnyima mgombea nafasi ya kushiriki katika uchaguzi kwa vile tu fomu yake haijajazwa vipengele vyote.

Nyalla aliondolewa kwenye uchaguzi na Kamati ya Uchaguzi ya TFF kwa maelezo kuwa si mtu makini anayeweza kutekeleza majukumu yake kikamilifu baada ya kushindwa kujaza Fomu namba 1 kipengele cha 15 kinachohusu malengo ya mgombea uongozi.

Kwa upande wa Nyaulingo ambaye aliondolewa kwa kukosa uzoefu uliothibitika kulingana na Ibara ya 29(3) ya Katiba ya TFF na Kanuni ya 9(3) ya Kanuni za Uchaguzi za TFF, Kamati ya Rufani imeamua ifuatavyo;

Kamati ya Rufani ya Uchaguzi imepokea sababu za rufani na imepata fursa ya kusikiliza hoja na maelezo kutoka kwa Mrufani juu ya sababu zake alizozitoa kupinga uamuzi wa Kamati ya Uchaguzi.
Mrufani alifafanua historia yake katika masuala ya michezo kuanzia alipokuwa anasema Chuo Kikuu kuanzia 2005-2009 na pia ushiriki wake kama mchezaji wa Rukwa United iliyowahi kushiriki Ligi ya Mkoa wa Rukwa na ligi nyingine za kitaifa.
Kwa kusoma maana ya ‘Familia ya TFF’ iliyoko kwenye utangulizi wa Katiba ya TFF, pamoja na Ibara ya 29(3) na 29(6) ya Katiba hiyo, Kamati imejiridhisha kuwa Mrufani ana sifa za kugombea uongozi wa Shirikisho na amekidhi kigezo cha sifa za ugombea.

Ameshiriki kwenye mchezo wa mpira wa miguu kama mchezaji na mtawala, hivyo kutimiza kigezo kilichohitajika cha ushiriki katika uongozi na utawala wa mchezo wa mpira wa miguu kwa muda usiopungua miaka mitano.

Kwa kuzingatia hayo, Kamati ya Rufani ya Uchaguzi inaruhusu rufani ya Mrufani. Uamuzi wa Kamati ya Uchaguzi umetenguliwa na Mrufani anapewa nafasi ya kushiriki katika uchaguzi.

Kuhusu Ayubu Nyenzi aliyeondolewa kwa kukosa uzoefu kwa mujibu wa Ibara ya 29(3) ya Katiba ya TFF na Kanuni ya 9(3) ya Kanuni za Uchaguzi za TFF, na pia kushindwa kuthibitisha uraia wake mbele ya Kamati ya Uchaguzi, Kamati ya Rufani katika uamuzi wake imesema;

Imepokea sababu za rufani na imepata fursa ya kusikiliza hoja na maelezo kutoka kwa Mrufani juu ya sababu zake alizozitoa kupinga uamuzi wa Kamati ya Uchaguzi.

Baada ya uchambuzi wa kina, Kamati imeona kuwa kulingana na maelezo yaliyotolewa na Mrufani na viambatanisho vilivyowasilishwa, Kamati haina shaka kuhusu uraia wake. Uthibitisho wa uraia unapaswa kufanywa kwa umakini na taasisi yenye mamlaka ya kiserikali kufanya hivyo.

Kamati pia imejiridhisha kupitia Fomu namba 1 iliyojazwa na kusainiwa na Mrufani kuwa kuanzia mwaka 2004 mpaka 2010, Nyenzi ameshika nyadhifa za utawala wa mpira wa miguu na hasa katika klabu ya Yanga, uzoefu unaomfanya kuwa na sifa ya kugombea nafasi ya uongozi katika TFF kulingana na Ibara ya 29(3) ikisomwa pamoja na Ibara ya 29(6).

Kwa kuzingatia hayo, Kamati ya Rufani ya Uchaguzi inaruhusu rufani ya Mrufani. Uamuzi wa Kamati ya Uchaguzi umetenguliwa na Mrufani atashiriki katika uchaguzi wa TFF kwa nafasi anayogombea.

7 October 2013

MVUA AU JUA UCHAGUZI LAZIMA OCT 27 :TENGA

Rais wa Shirikisho la Mpira wa Miguu Tanzania (TFF), Leodegar Tenga amewahakikishia Watanzania kuwa uchaguzi wa kupata Kamati mpya ya Utendaji ya shirikisho utafanyika Oktoba 27 mwaka huu kama ilivyopangwa.

“Wazungu wanasema ije mvua au jua, uchaguzi utafanyika. Isipokuwa tunachotaka kuhakikisha ni kuwa unakuwa uchaguzi huru na wa haki,” amesema Rais Tenga wakati akizungumza na waandishi wa habari kwenye ofisi za TFF leo mchana (Oktoba 7 mwaka huu).

Amesema mchakato unakwenda vizuri kilichobaki ni revision (mapitio) na rufani, masuala ambayo yako mbele ya Kamati ya Rufani ya Maadili na Kamati ya Rufani ya Uchaguzi.

Rais Tenga amesema lengo la hatua hizo si kuzuia watu wasigombee kwani ni lazima mambo ya msingi ikiwemo sifa za wagombea yaangaliwe, lakini kwenye haki ni lazima kuhakikisha inatendeka hata kama ni kwa mtu mmoja.

Mchakato wa uchaguzi ulivutia waombaji 58 ambapo watatu wamekata rufani Kamati ya Rufani ya Uchaguzi kupinga kuondolewa na Kamati ya Uchaguzi wakati wengine wanane masuala yao yamepelekwa Kamati ya Rufani ya Maadili kwa njia ya mapitio (revision) ili kupata mwongozo wa utekelezaji.

Mwongozo huo umeombwa na Sekretarieti ya TFF kwa Kamati ya Rufani ya Maadili kwa vile Kamati ya Maadili iliwaona waombaji wanane wa uongozi waliofikishwa mbele yake kwa makosa ya kimaadili kutokuwa na hatia, lakini wakati huo huo ikitambua kuondolewa kwao kwenye kinyang’anyiro cha uchaguzi kulikofanywa na Kamati ya Uchaguzi.
wakati huo huo 
MRADI WA FOOTBALL FOR HOPE KUFUNGULIWA OKTOBA 13
Mradi wa Football for Hope kusaidia watoto na wasiojiweza kupitia mpira wa miguu uliofadhiliwa na Shirikisho la Kimataifa la Mpira wa Miguu (FIFA) mkoani Iringa utafunguliwa rasmi Oktoba 13 mwaka huu.
FIFA hutoa mradi huo kwa baadhi ya nchi kwa kuzingatia mambo mbalimbali ikiwemo utawala bora, lakini kwa kupitia taasisi zisizo za kiserikali (NGOs) ambapo kwa Tanzania umepatikana kupitia taasisi ya Iringa Development of Youth, Disabled and Child Care (IDYDCC).

Rais wa TFF, Leodegar Tenga ameishukuru FIFA kwa msaada huo, kwani ni mkubwa na kuongeza kuwa ni matumaini yake utatumika kwa lengo lililopangwa.

Amesema mradi huo wa FIFA ambao ni wa kusaidia watoto kielimu na wasiojiweza kwa kupitia mpira wa miguu haukupita moja kwa moja TFF ni mzuri kwani moja ya mambo uliofanikisha ni kuwepo jengo na sehemu ya watoto kucheza.

Ni wastani wa nchi kumi tu duniani kwa mwaka zinapata mradi huo kutoka FIFA, jambo ambalo Rais Tenga amesema linachangiwa pia na uhusiano na ushirikiano uliopo kati ya Tanzania na shirikisho hilo.

1 October 2013

RUFANI KAMATI YA MAADILI MWISHO OKT 2

 
Wakati walalamikiwa waliofikishwa kwenye Kamati ya Maadili ya Shirikisho la Mpira wa Miguu Tanzania (TFF) wakiwa wameshapokea uamuzi dhidi yao kwa maandishi, mwisho wa kukata rufani Kamati ya Rufani ya Maadili ni kesho (Oktoba 2 mwaka huu).

Walalamikiwa wote saba waliohudhuriwa mashauli dhidi yao; Kamwanga Tambwe, Nazarius Kilungeja, Omar Abdulkadir, Richard Rukambura, Riziki Majala, Shaffih Dauda na Wilfred Kidao wamepokea uamuzi wa Kamati hiyo inayoongozwa na Jessie Mnguto.

Kwa mujibu wa Kanuni za Maadili, kwa ambao hawakuridhika na uamuzi huo wanatakiwa kukata rufani Kamati ya Rufani ya Maadili inayoongozwa na Jaji Mstaafu Stephen Ihema ndani ya siku tatu zinazomalizika kesho.

Rufani ziwasilishwe kwa Katibu Mkuu wa TFF kabla ya saa 10 kamili jioni. Kwa mujibu wa Kanuni ya 74 (1) na (2) ya Kanuni za Maadili, rufani zikionesha sababu za kufanya hivyo zinatakiwa kuwasilishwa ndani ya siku tatu kwa njia ya posta (registered post or dispatch or courier service) kwa Sekretarieti.

Vilevile inatakiwa rufani inatakiwa kuambatanishwa risiti ya malipo ya ada ya rufani. Ada ya rufani ni sh. milioni moja.

lisungu_chisara@yahoo.com

TUTUMIE HABARI YOYOTE YA MICHEZO, BURUDANI TUTAZICHAPISHA

TANGAZA KWA MFUMO HUU


MAHUDHURIO YA WASOMAJI KIMATAIFA

free counters

Followers