Shirikisho la Soka duniani Fifa litafanyia uchunguzi kauli iliyotolewa na aliyekuwa mwenyekiti wa Chama cha Soka cha England (FA) Lord Triesman inayohusu kuwepo harufu ya "rushwa" katika mchakato wa kupata nafasi ya kuandaa Kombe la Dunia mwaka 2018.
Fifa yamchunguza Lord Trriesman
Triesman alisikika katika gazeti moja la udaku akitamka kwamba Hispania huenda ikajitoa katika kinyang'anyiro cha kuwania nafasi hiyo iwapo mshindani mwengine Urusi itaisadia kuwahonga waamuzi katika fainali za mwaka huu za Kombe la dunia.
Fifa pia imeiandikia FA ikitaka ipatiwe ripoti ya sakata hilo la Triesman.
FA imeahidi kutoa ushirikiano wa hali ya juu kwa Fifa, ambapo kanuni zake zinakataza nchi inayowania kuandaa kutoa matamshi kuhusu wapinzani wao katika kinyang'anyiro.
Taarifa rasmi ya Fifa imesema: "Fifa inathibitisha Katibu wake Mkuu Jerome Valcke ameiomba kamati ya Maadili kuchunguza tuhuma za matamshi yaliyotolewa na Lord Triesman ikihusishwa na mchakato wa kupata nafasi ya kuandaa Kombe la Dunia mwaka 2018 na 2022.
"Zaidi ya hapo, Fifa imeandika barua kwa Chama cha Soka cha England kukitaka kitoe ripoti kamili juu ya suala hilo na nafasi ya Lord Triesman.
"Fifa haitatoa tamko lolote zaidi kuhusiana na suala hilo hadi litakaposhughulikiwa na Kamati ya Fifa ya Maadili."
Kaimu Mkuu wa FA, Alex Horne, amejibu hoja hizo za Fifa kwa kusema: "Ni muhimu kwamba sasa tunaweza kushirikiana na Fifa na sehemu nyingine za dunia kwa wakati huu ambapo tumedhamiria kutafuta nafasi ya kuandaa Kombe la Dunia mwaka 2018. Suala la umbeya na mambo ya kipuuzi hayana nafasi."
Triesman alilazimika kujiuzulu uenyekiti wa kamati inayosimamia England kutafuta nafasi ya kuandaa Kombe la Dunia mwaka 2018 baada ya kurekodiwa kwa siri akituhumiwa kutoa matamshi yenye taarifa nyeti kwa mwandani wake wa zamani.
Tuhuma hizo ni pamoja na madai kwamba Hispania na Urusi, mahasimu wawili wanaowania kuandaa Kombe la Dunia mwaka 2018, walikuwa na njama kuwahonga waamuzi katika fainali za mwezi ujao za Afrika Kusini, kama sehemu ya jitahada za kushinda haki ya kuandaa Kombe la Dunia.
No comments:
Post a Comment