Siku moja kabla ya mwanariadha Caster Semenya wa Afrika ya Kusini, kushiriki mbio za mita 800, kocha wake anasema hajafikia viwango vilivyomuezesha kushinda medali ya dhahabu.
Kocha Michael Seme amesema Semenya analenga muda wa dakika mbili na sekunde nne hapo kesho kwenye mashindano ya Lappeenranta.
Hii itakuwa mara ya kwanza kwa mkimbiaji huyu kushiriki mashindano ya aina yoyote katika kipindi cha mwaka mmoja.
Kwa muda mrefu Semenya amekuwa akifanyiwa uchunguzi kuhusu jinsia yake iliyozusha ubishi.
Kocha wa mwanamke huyo amesema Semenya bado hajapata uwezo wa kufikia rekodi aliyoiweka mjini Berlin akiwaacha mbali wapinzani wake.
Hata hivyo wadadisi wanahisi kuwa Semenya atawashinda wapinzani wake kwenye mashindano yanayofanyika nchini Finland akiwemo Olga Yekimenko kutoka Ukraine ambaye ana muda ulio chini ya kasi ya Semenya kwa sekunde tano.
Kocha Seme amesema kuwa nia yake ni kumtayarisha Semenya aweze kufikia kiwango cha kumuezesha kushinda mbio za mita 800 kwenye mashindano ya riadha ya Jumuia ya Madola mjini New Delhi huko India.
Katika mahojiano na gazeti la nchini Finland, llta-sanomat, Semenya amesema anahitaji hadi mashindano 12 kuweza kufikia kiwango chake cha kabla ya kusimamishwa kushiriki mashindano ya riadha.
Kujitokeza kwa Semenya kwenye mashindano haya yanyofanyika kwenye uwanja wa Kimpinen kumevutia vyombo vya habari kutoka kila pembe ya dunia.
Kwa kawaida mashindano haya hufanyika kwa ukimya. Semenya aliachwa nje ya kikosi cha Afrika ya Kusini kitakachoshiriki mashindano ya Afrika mwezi huu nchini Kenya. BBC SWAHILI UMELEZWA
No comments:
Post a Comment