Viongozi waandamizi wa Nchi mbali mbali walishiriki kuzipa moyo wa ushindani timu zao, hapa ni Balozi wa Tanzania katika Uingereza Mhe Peter Kallaghe, akiwa na Mkurugenzi wa maendeleo ya michezo Leonard Thadeo, pamoja nao ni Naibu Balozi, Bw Chabanga |
MWISHO wa Michezo ya 30 ya Olimpiki iliyofayika London, Uingereza,
ndio mwanzo wa michezo ya 31 itakayofanyika Rio de Janeiro, Brazil mwaka
2016.
Kati ya mambo yaliyojitokeza kwenye michezo ya mwaka huu, ni
wenyeji kutumia vyema rasilimali zao na kufikia kilele cha mafanikio ya
miaka 104.
Ni kweli kwamba Marekani na China zimefanya vizuri kwa wingi wa medali kwa ujumla, zikiwamo za dhahabu.
Ni kweli pia Michael Phelps wa Marekani ametangazwa kuwa mwanamichezo mahiri zaidi wa muda wote katika Olimpiki kwa wingi wa medali zake za dhahabu.
Lakini kama kuna la kujifunza katika mageuzi ya michezo kwa nchi
kwa ujumla, na ufanisi wa mchezo mmoja hadi mwingine, Uingereza ni somo
tosha.
Fahari ya taifa hili kwa maandalizi mazuri, sherehe bora za ufunguzi na murua za ufungaji michezo ni heshima yao kama waandaaji.
Mchezoni, wanamichezo wake wengi hawakuwa na ajizi. Walitumia vyema
mafunzo ya makocha na jitihada binafsi katika vitendo, wakapata medali.
Kocha na Mkurugenzi wa Mafunzo wa Chama cha Mbio za Baiskeli
Uingereza, David Brailsford, ambaye pia ni kocha wa timu hiyo, amepata
mafanikio makubwa.
Katika Olimpiki hii ameshuhudia medali 12, nane kati ya hizo zikiwa
za dhahabu. Ni huyu pia aliyechochea ushindi wa Bardley Wiggins katika
mashindano ya Tour de France, akiwa meneja mkuu wa Team Sky.
Daima timu au mchezaji anapofika kileleni changamoto zinazowakabili
huongezeka, maana wanakuwa wameshajiwekea kipimo cha juu kisichotakiwa
kushuka tena.
Wakati mawazo na mipango ya wadau vikielekea Rio, Uingereza na timu
yake – Team GB, wana mtihani wa kushikilia kiwango chao au kukipandisha
juu tayari kwa michezo ijayo nchini Brazil.
Tayari matumaini yamekuzwa katika michezo hii, ambapo nchi imevuna
medali medali 65. Wana dhahabu 29, fedha 17 na shaba 19. Haijapata
kutokea tangu mwaka 1908.
Tayari wanamichezo wengine wanaangalia jinsi ya kufuata nyayo za
hao wa mbio za baiskeli na wapiga makasia waliokusanyia nchi medali
tisa, zikiwamo nne za dhahabu.
Mwalimu Brailsford anasema Uingereza inatakiwa kukaza kamba kwa
kuhakikisha hawapotezi kanuni walizotumia kufikia hesabu nzuri ya jumla
iliyowaweka juu kiasi hicho – nafasi ya tatu kwa ujumla.
“Mambo yamekwenda vizuri, ugharimiaji umeleta tofauti kubwa katika
jinsi nchi ilivyofanya vizuri kwenye michezo. Inaendeshwa na kusimamiwa
vizuri. Inafanya kazi.
“Kinachonitatiza kidogo ni hili suala la kutaka kubadilisha mfumo.
Wanakuja watu wanataka kuanza mambo upya kwa mawazo tofauti katika kila
kitu,” anasema.
Maoni yake ni kwamba njia ambazo Uingereza imeanza kufuata
zinatakiwa kuenziwa. Hataki kuona wanasiasa wakiingilia kuelekeza cha
kufanya, wakati tayari mafanikio yameanza kuonekana.
Badala yake, anaona dalili za mafanikio zaidi zitatokana na vyama
vya michezo tofauti kushindana katika kila kimoja kujaribu kuongoza
michezo kisomi.
“Kwa kifupi ni kwamba mfumo huu unafanya kazi, tusipouingilia na kuuvuruga, utaendelea kufanya kazi.
“Huwezi kuwekeza kwenye michezo kama tunavyofanya uache
kufanikiwa…mbaya ni kugutuka na kufanya mabadiliko yasiyo na msingi. Kwa
hiyo wanasiasa kaeni mbali, elekezeni fedh kwenye michezo, ziende kwa
wakurugenzi,” anasisitiza.
Kwa watakaosikiliza ushauri bila shaka wataona mafanikio, kama aliyowezesha Brailsford kwenye Michezo ya 30 ya Olimpiki.
Michezo hiyo ya London 2012 ilianza kwa sherehe ya ufunguzi.
Mashujaa saba wa Olimpiki wa Uingereza wa miaka iliyopita walikabidhi
mienge yao kwa kizazi kingine –wanamichezo chipukizi saba wanaotabiriwa
kuwa nyota siku zijazo.
Baada ya hapo waliwasha moto kwenye Mwenge mkubwa katika Uwanja wa Olimpiki.
Mmoja wa chipukizi hao alikuwa kijana mwenye umri wa miaka 18 – Katie Kirk.
Huyu alikuwa kwenye timu iliyopata ushindi wa kwanza katika mbio za
kupokezana vijiti katika michuano ya Ubingwa wa Ulaya mwaka jana.
Sasa amenuia, na yupo katika mipango ya kuhamia kwenye mbio za mita 800 kwa ajili ya michezo ijayo ya Olimpiki.
Katie anayetoka Belfast, anasema kwamba mfano uliowekwa na wana
Team GB waliopata medali ni hamasa tosha kwake kufanya kazi kwa nguvu
zaidi kulifikia lengo lake.
“Hii inakuhamasisha kuongeza jitihada kwa sababu unajua unataka uwepo na ushindane katika ngazi hiyo.
“Medali zote zilizopatikana zina maana kubwa mno, kwa sababu
ukifuatilia waliozipata, utaona jinsi walivyokuwa wakipiga hatua moja
baada ya nyingine.
“Nakumbuka kumtazaa Mo Farah miaka michache iliyopita, alikuwa
akikimbia vyema lakini hakuwa vizuri kama alivyo leo. Hii inaonesha
kwamba ukiongeza bidii utafikia ngazi unayotaka,” anasema binti huyo.
Katie alichaguliwa na Dame Mary Peters, mwanariadha pekee alyepata
medali ya dhahabu katika Olimpiki ya mwaka 1972 iliyofanyika Munich.
Mchezo alioshindia dhahabu, leo hii hujumuisha hatua mbalimbali,
zikiwamo riadha, kuruka na kulenga shabaha. Ndio mchezo alioshinda
Jessica Ennis.
“Nilikuwa na kocha mmoja, aliyezoea kukandamiza mkono wangu kwa
nguvu huku akisema; ‘umefanya vyema, lakini ungeweza kufanya vizuri
saidi’.
“Lakini leo wachezaji wana wataalamu wa saikolojia, wana wataalamu
wa mifumo ya kibayolojia…kila aina ya wataalamu kwenye masuala ya afya,
tofauti kabisa na enzi zetu,” anasema Peters.
“Ukipata watoto katika miaka yao ya awali – China wanawaanzia katika umri wa miaka mitatu – unaweza kuwajenga kuwa mabingwa.
“ Lakini si kila mtu anataka kufuata njia hiyo, wengine wanataka kuwa na nyakati nyingi za kupumzika na furaha zaidi.
“Hata hivyo, hakuna jambo la furaha zaidi ya unavyojisikia baada ya
kushinda, umesimama kwenye jukwaa na unasikiliza wimbo wa taifa
unapigwa,” anatoboa siri hiyo.
Gemma Gibbons alitwaa medali ya fedha kwenye judo na mwanatimu mwenzake, Karina Bryant siku iliyofuata akapata shaba.
Kilichotokea baada ya hapo ni kwamba ushindi ulichochea mapenzi
kwenye mchezo huo. Mara watu 5,000 wakaomba kujiunga na klabu mpaka
tovuti ikalemewa na kushindwa kufanya kazi kutokana na wingi wa waombaji
waliokuwa mtandaoni.
Wiki moja baadaye, Gemma alikuwa Hyde Park akionesha medali yake kwa watoto waliokuwa wamepigwa na butwaa wakiwa mazoezini.
Michezo inayochukuliwa kuwa ni midogo inahitaji kutangazwa na
ikitokea kuna ushindi wa medali, basi huvutia wachezaji wapya wanaoweza
kuwa nyota wa siku zijazo.
Ofisa Mtendaji Mkuu wa Judo Uingereza, Andrew Scoular alikuwa na
haya ya kusema: “Sasa watu wameona wanamichezo wanashinda medali kwenye
Michezo ya Olimpiki, upenzi unaanza kuwepo.
“Ukizingatia idadi ya watu wanaoongezeka kila mara na mchezo
wenyewe unavyokua, lazima kutazama kwa makini, kuibua vipaji na kuvikuza
kwa ajili ya Rio na baada ya hapo,” anasema Scoular.
Wanaamini kwamba siku moja watakuwa katika mafanikio ya wenzao wa
mbio za baiskeli na upigaji makasia, kwa kutawala michezo mingine.
Gemma alisema: “Nadhani judo ya Uingereza inaweza kuwa hivyo. Ni
wazi tuna safari ndefu baso, lakini nahisi hii tayari ni hatua ya
kwanza. Tukiipiga ipasavyo, katika miaka minane au 12, tutakuwa kama wa
mbio za baiskeli.”
No comments:
Post a Comment