Timu ya kandanda ya Mexico imewashangaza mashabiki wa
mchezo huo kwa kuichapa Brazil kwenye fainali ya Kombe la Olimpiki
katika uwanja wa Wembley mjini London.
Oribe Peralta aliipatia Mexico bao la kwanza ikiwa ni sekunde 29 baada ya kipenga cha kuanza mchuano kupulizwa.Peralta litumia fursa iliyotokana na kosa la beki wa Brazil kuchezea katika nusu ya uwanja kwa upande wa Brail na kuikandika Brazil bao la haraka lililozipeleka pande hizi hadi mapumziko kwa hesabu ya 1-0 kwa Mexico.
Mshambuliaji huyo huyo alirudi kutikisa nyavu za Brazil mnamo dakika ya 75 kwa mpira wa kichwa.
Brazil ilipata bao lake la kufutia machozi kupitia mshambuliaji Givaldino Hulk zikisalia dakika kama tatu hivi kufikia mwisho wa mechi lakini Mexico ikashikilia mabao yake mawili hadi kipenga cha mwisho.
Hivyo basi historia inabaki pale pale kwa Brazil kuondoka mashindano haya ya Olimpiki bila medali ya dhahabu ingawa itaondoka na fedha.
Jumla ya watu 86,162 wameshuhudia pambano hili ikiwa ni idadi kubwa kuwahi kuhudhuria mechi yoyote kwenye mashindano haya ya Olimpiki ya London 2012. Jumla ya watu milioni 2,186,930 wamehudhuria mashindano ya mpira ya wanawake na wanaume kwenye Olimpiki hizi.
No comments:
Post a Comment