HABARI MPENZI MWANAMICHEZO KARIBU KATIKA KURASA HII MAHSUSI KWA HABARI ZA MICHEZO PIA UNAWEZA KUTANGAZA BIASHARA YAKO HAPA KWA BEI NAFUU ZAIDI KWA MUDA MREFU ZAIDI WASILIANA NASI KWA NAMBA +255713 15 33 48

3 August 2012

Waliobaki wataibeba Tanzania Olimpiki?

Na Israel G Saria Lonndon
Michezo ya 30 ya Olimpiki imetimiza wiki moja jijini London, nchi mbalimbali zikijizolea medali za dhahabu, fedha na shaba.
China na Marekani zilikuwa zimejizolea wastani wa medali 15 za dhahabu hadi Alhamisi mchana, huku majaliwa ya Tanzania yakiwa gizani.
Wenyeji Uingereza walioanza kwa kuchechemea, wakaelekea kuchoka kwa kukosa medali za dhahabu, waliingia siku ya tano kwa furaha, kwani wachezaji walikata kiu yao.
Baada ya kupata medali mbili za dhahabu Jumatano katika mbio za baiskeli na kupiga makasia, dakika tano za Alhamisi zilishuhudia wenyeji hawa wakizoa dhahabu mbili na fedha moja.
Linapokuja suala la kuzungumzia timu za nyumbani Afrika, wengi wanatafuta kimbilio Afrika Kusini, kama vile kutangaza au kuandika kwamba Afrika Kusini imelinyanyua bara la Afrika kwa kupata medali tatu za dhahabu.
Israel G Saria akiwa na Zakia Mrisho London Uingereza katika mashindao ya olimpik       


Zakia Mrisho, mkimbiaji mahiri, ni tegemeo kubwa la kufanya vizuri katika mbio
Pamoja na chenga tunazojaribu kupiga, ni vyema tukaliweka wazi suala lenyewe – kwamba kwa Tanzania hadi sasa haijapata medali yoyote na wachezaji wake watatu wameshayaaga mashindano.
Ukweli ni kwamba wawili kati ya watatu waliotolewa walionesha kiwango kibovu kwenye ndondi na kuogelea, wakati mmoja anaweza kueleweka kwa kushindwa.
Mhanga wa karibuni kabisa na ambaye hakuonyesha kiwango cha juu ni Magdalena Moshi. Msichana huyu alishiriki kuogelea kwa freestyle mita 100 na kumaliza akiwa wa mwisho.
Magdalena anayesoma Australia ambako pia hushiriki kuogelea kwenye moja ya klabu za huko, aliaga michezo hiyo Jumanne mchana, alipokubali wenzake sita kumzidi kete kwenye mashindano ya mchujo.
Huyu ndiye mwanamke wa kwanza Tanzania kushiriki Olimpiki, na alijitokeza kwa mara ya kwanza Beijing, China mwaka 2008 na hii ni mara ya pili.
Safari zote hizi anaondoka bila medali, ambapo Jumanne katika Aquatic Centre, Magdalena alitumia dakika 1:04:93 kumaliza shindano lake.
Katika mpangilio wa shindano hilo, Jade Ashleigh Howard wa Zambia aliongoza kwa kutumia sekunde 59:35.
Huyo alifuatiwa na Baean Jouma wa Syria katika nafasi ya pili wakati ile ya tatu ilishikwa na Karen Riveros wa Paraguay. Magdalena hakuweza walau kuambulia nafasi ya nne, kwani ilinyakuliwa na Britany Van Lange wa Guyana.
Bado bendera ya Tanzania haikuonekana na watu kukata tamaa, kwa sababu aliyeshika nafasi ya tano ni raia wa Madagascar, Esellah Fils Rabetsara. Kilichowafanya watu wajue huyu wetu alikuwa wa mwisho, ni nafasi ya sita kubandikwa bendera ya Sri Lanka, kwa ajili ya Reshika Amali Udugampola aliyempiku pia Magdalena kwa kwenda kasi ya dakika 1:02:39.
Watanzania walio London, sawa na walio nyumbani Tanzania na maeneo mengine walikatishwa tamaa, kwani ama walikuwa wakitumia mitandao jamii kujua matokeo au kutoa salamu za heri kabla ya Magdalena kuogelea.
Matokeo hayo yalikuja baada ya mwogeleaji mwingine wa Tanzania, mvulana Ammaar Ghadiyali kujitutumua lakini akakosa nafasi moja kuingia kwenye awamu ya pili, hivyo kutolewa katika mchujo.
Ghadiyali hakuwa kwenye orodha ya awali ya washiriki, kwa vile hakuwa ameteuliwa wala kuidhinishwa na vyama husika.
Hata hivyo, alikuwa akifanya mazoezi kivyake hadi nafasi ilipopatikana kutokana na baadhi ya nchi kujitoa ushiriki wao au wa baadhi ya waogeleaji wao wanaume, ndipo akapewa huyu.
Ghadiyali hakuwa kambini kwa muda mrefu Uingereza kama wenzake waliokaa karibu mwezi mmoja sasa. Katika mazingira hayo, naweza kusema kushindwa kwake kunaeleweka.
Pamoja na kujitahidi kwake, ni wazi hakuwa ametulia vizuri kistamia na zaidi kisaikolojia, hivyo angekuwa tayari na maandalizi na ratiba ya kueleweka, naamini tungeweza kuwa tunazungumza mengine hivi sasa.
Kwa vile ni kijana mdogo mwenye umri wa miaka 15, anatakiwa kupewa kipaumbele katika maandalizi na kushiriki mashindano mengine, maana ataipeperusha vizuri bendera ya Tanzania.
Ghadiyali alitumia dakika 1:01:07 wakati wawili waliomtangulia na kufuzu ni Soumare Mamadou wa Mali aliyetumia sekunde 57:32 na Husam Ahmed wa Maldives aliyetumia sekunde 57:53.
Niliandika kuhusu ndoto za Olimpiki za Tanzania kuzimika, kwa sababu mbalimbali.
Baadhi ya sababu hizo ni kukosa uongozi bora unaosababisha kutoibua vipaji, hivyo wale waliostahili kwa mfano kuwa London leo hii wakitamba na kuitangaza vyema Tanzania hawapo.
Dhihirisho la hayo lilionekana alipoanza Mtanzania wa kwanza aliyefuzu na kupitishwa kuja kushindana Olimpiki.
Huyo alikuwa Selemani Kidunda, ambaye pia alikuwa bondia pekee kwenye timu. Jumapili ile aliyopanda ulingoni kuchuana na Vasilii Belous wa Moldova, ilikuwa chungu kwa Watanzania.
Walioshuhudia watakubaliana nami ukosefu wa kipaji ndani yake, stamina na uwezo, kwa jinsi alivyomwachia mpinzani wake kupata pointi kirahisi kwa kumpiga maeneo yanayohesabiwa pointi.
Kidunda ambaye katika hali ya kushangaza kocha wake, Michael Changarawe alibaki Tanzania.
Tena wakati bondia akipanda ndege Dar es Salaam kuja Heathrow, yeye Changarawe alikwenda Mwanza kupumzika kabisa!
Hali ilikuwa ngumu tangu mwanzo wa mchezo, maana Belous katika pambano hilo la uzito wa kilo 69, alimshindilia ngumi mfululizo Mtanzania wetu, na mapema tu alikuwa ameshajipatia pointi 26.
Hadi pambano linaelekea mwisho, kila mmoja alijua mshindi angekuwa Belous, majaji wakamgawia pointi 20 dhidi ya saba za Kidunda. Katika hali hiyo, hakuna wa kulaumu, isipokuwa bondia mwenyewe, kocha wake au wahusika waliompitisha.
Katika muda uliobaki, wapeperusha bendera ya Tanzania waliobaki, ambao ni wanariadha wanne, wanatakiwa kuongeza mazoezi kama wanataka kurudi na chochote nyumbani.
Japokuwa wenzao wametolewa, hawa wanajivunia rekodi nzuri kwenye mashindano mbalimbali. Licha ya hivyo, wamekuwa wakiungwa mkono na wadau na kuhakikishiwa mahitaji yote muhimu.
Kwa hiyo macho na masikio ya Watanzania yataelekezwa kwa mwanariadha Zakhia Mrisho ambaye Jumanne ijayo atashiriki mbio za mita 5,000.
Zakhia alishiriki pia Olimpiki ya Beijing alikoshika nafasi ya nne. Hata hivyo ana kumbukumbu ya ushindi wa Michuano ya Adidas ya kilometa tano yaliyofanyika Jamhuri ya Czech mwaka 2010.
Mategemeo mengine ya Tanzania ni Faustine Musa, Mohamed Msenduki na Samson Ramadhani. Zamu yao ni Agosti 12
Musa alianza riadha akiwa shule ya msingi na sasa ana meneja wake nchini Ujerumani anayemsaidia kupata mbio za kushiriki na kukuza kipaji chake.
Mohamed Msenduki aliwahi kushinda Marathon ya Buoenos Aires, Argentina mwaka 2009, kwa hiyo huenda akafanya kweli atakachuana na wengine siku hiyo.
Samson Ramadhani si mgeni kwenye marathon. Ameshashinda medali ya dhahabu kwenye Michzo ya Jumuiya ya Madola ya Australia iliyofanyika mwaka 2006, ambapo alitumia dakika 2:11:29.
Ameshiriki mashindano mengine kadhaa, yakiwamo
tano katika Marathon ya London na wa 15 kwenye mashindano ya ubingwa wa dunia jijini Paris, Ufaransa.
Alishiriki Olimpiki ya mwaka 2004 akawa wa 40 katika marathon na ile iliyofuata Beijing alikuwa wa 55. Hata hivyo amefanya vizuri kwenye mashindano mengine mbalimbali, na anatarajiwa kutumia uzoefu wote huo jijini London safari hii.



No comments:

Post a Comment

lisungu_chisara@yahoo.com

TUTUMIE HABARI YOYOTE YA MICHEZO, BURUDANI TUTAZICHAPISHA

TANGAZA KWA MFUMO HUU


MAHUDHURIO YA WASOMAJI KIMATAIFA

free counters

Followers