Ligi Daraja la Kwanza
(FDL) kuanzia msimu huu wa 2012/2013 itakuwa na timu 24 kutokana na mabadiliko
ya mfumo wa mashindano yaliyofanywa na Shirikisho la Mpira wa Miguu Tanzania
(TFF).
Kamati ya Utendaji ya
TFF ilikutana Julai 29 mwaka huu ambapo pamoja na mambo mengine ilifanya
mabadiliko ya mfumo wa mashindano ikiwemo FDL kuchezwa kwa mtindo wa nyumbani
na ugenini badala ya ule wa awali wa vituo.
Kutokana na
mabadiliko hayo, timu za FDL zitagawanywa katika makundi mawili ya timu 12 kila
moja kutokana na ukaribu wa kanda na kucheza kwa mtindo wa nyumbani na ugenini. Timu ya kwanza kutoka
kila kundi itapanda kucheza Ligi Kuu msimu unaofuata wakati ya tatu
itakayoungana na hizo mbili itapatikana kwa mechi za nyumbani na ugenini kwa
timu zilizoshika nafasi ya pili katika kila kundi. Ili kufikisha idadi
ya timu 24 kwenye FDL, Kamati ya Utendaji ya TFF kwa kuzingatia mapendekezo ya
Kamati ya Mashindano imeamua timu tatu za juu kwenye Ligi ya Taifa kutoka vituo
vyote vitatu vya ligi hiyo zimepanda daraja.Sasa timu 24 za FDL
ni Ashanti United (Dar es Salaam), Burkina Moro (Morogoro), Green Warriors (Dar
es Salaam), Kanembwa JKT (Kigoma), Kurugenzi Mafinga (Iringa), Majimaji
(Ruvuma), Mbeya City (Mbeya), Mkamba Rangers (Morogoro), Mlale JKT (Ruvuma) na
Morani (Manyara).
Nyingine ni Moro
United (Dar es Salaam), Mwadui (Shinyanga), Ndanda (Mtwara), Pamba (Mwanza),
Polisi (Arusha), Polisi (Dodoma), Polisi (Iringa), Polisi (Mara), Polisi
(Tabora), Rhino Rangers (Tabora), Small Kids (Rukwa), Tessema (Dar es Salaam),
Transit Camp (Dar es Salaam), Villa Squad (Dar es Salaam)
Timu nne zitashuka
daraja kurudi Ligi ya Mkoa. Timu hizo ni mbili zilizoshika nafasi za mwisho kwa
kila kundi. Timu nne zitakazopanda kucheza FDL zitapatikana kwa mchujo
utakaohusisha mabingwa wa mikoa.
Kwa mfumo huo mpya wa
mashindano, ligi za mikoa zitakazosimamiwa na kuendeshwa na vyama vya mpira wa
miguu vya mikoa zinatakiwa kuwa na timu zisizopungua 16 na zisizozidi 20. Ligi
za mikoa pia zitachezwa mwaka mzima kwa mikondo miwili (nyumbani na ugenini).
Ligi ya mkoa
itashusha timu mbili na kupandisha nyingine mbili kutoka ligi ya wilaya. Ligi
za wilaya zitakazosimamiwa na kuendeshwa na vyama vya mpira wa miguu vya wilaya
zinatakiwa kuwa na timu zisizopungua 10 na zisizozidi 20.
Kwa wilaya zenye timu
zaidi ya 20, chama husika cha mpira wa miguu kitapanga utaratibu wa kuzichuja
kwa mashindano ili kupata zile bora 20 zitakazocheza ligi rasmi ya wilaya.
Mabingwa wa wilaya
katika mkoa husika watacheza mechi za kuchujana (play offs) ili kupata timu
mbili zitakazopanda daraja kucheza ligi ya mkoa husika.
Kutokana na
mabadiliko hayo ya mfumo wa mashindano, sasa madaraja rasmi ya ligi ni Ligi
Kuu, Ligi Daraja la Kwanza, Ligi ya Mkoa (Ligi Daraja la Tatu) na Ligi ya
Wilaya (Ligi Daraja la Nne).
TFF inasisitiza kuwa
kwa mujibu wa kalenda yake ya matukio, kipindi cha usajili wa wachezaji kwa
madaraja yote ni kimoja, na ligi zitachezwa kwa wakati mmoja.
Usajili wa hatua ya
kwanza ni kuanzia Juni 15 hadi Agosti 10 mwaka huu wakati kipindi cha pili cha
usajili ni Agosti 21 hadi Septemba 4 mwaka huu. Usajili wa dirisha dogo ni
Novemba 15 hadi Desemba 15 mwaka huu.
Ligi kwa madaraja
yote zitaanza Septemba. Ligi Kuu itaanza Septemba Mosi mwaka huu, Ligi Daraja
la Kwanza ni Septemba 15 mwaka huu, Ligi ya Mkoa na ile ya Wilaya zenyewe
zitaanza Septemba 8 mwaka huu.
Mechi za kufungua
msimu kwa madaraja yote (Ngao ya Jamii) ambazo kwa sasa zinakutanisha bingwa na
makamu bingwa zitachezwa Agosti 25 mwaka huu wakati michuano ya Kombe la FA
itaanzia wilayani Septemba 24 mwaka huu.
No comments:
Post a Comment