Ricky Hatton, bondia wa Uingereza ambaye zamani
alikuwa ni bingwa wa dunia katika viwango viwili vya uzani tofauti,
inaelekea huenda leseni yake ya kurudi katika ngumi ikaidhinishwa hivi
karibuni.
Hatton, mwenye umri wa miaka 33, alihudhuria kikao cha bodi ya ngumi, British Boxing Board of Control (BBBoC), mjini Cardiff, siku ya Jumatano, na anatazamiwa kuitisha mkutano na waandishi wa habari Ijumaa.
Katibu
mkuu wa bodi, Robert Smith, aliielezea BBC kwamba: "Leseni yake
atarudishiwa, mara tu baada ya kukaguliwa hali yake ya afya.
"Alizungumza vyema, anaonekana kuwa mwenye afya nzuri, na angelipenda kwa mara nyingine kushangiliwa."
Hatton, ambaye alibandikwa jina la utani 'The Hitman', yaani 'mgongaji',
hajawahi kupigana tena tangu aliposhindwa kwa KO katika raundi ya pili,
alipotandikana na Manny Pacquiao mwezi Mei, mwaka 2009.
Mwaka 2010, bodi hiyo ya ngumi ilimpokonya Hatton leseni, kufuatia madai ya kutumia dawa ya kulevya ya cocaine.
"Anaonekana yuko katika hali nzuri kabisa, hana shida yoyote, na inaelekea hana matatizo yoyote," alielezea Smith.
"Kutokana na matamshi yake, inaelekea ametulia
vyema na familia yake. Tayari ameshapitia ukaguzi fulani wa kimatibabu,
na tumo katika kuhakikisha anakamilisha utaratibu mzima."
No comments:
Post a Comment