Fabregas: Narudi Arsenal
*Asema akitoka Barca ni Emirates tu
Nahodha wa zamani wa Arsenal, Cesc Fabregas anayekipiga Barcelona ya Hispania, amedokeza uwezekano wa kurudi Emirates.
Fabregas amesema kwa sasa anafurahia mambo yalivyo Nou Camp, lakini ikiwa ataondoka, chaguo lake la kwanza ni Arsenal.
Kocha wa Arsenal, Arsene Wenger alisema mwezi uliopita kwamba anadhani ipo siku Fabregas atarudi kuchezea klabu hiyo ya kaskazini mwa London.
Kungo huyo aliwaacha Washika Bunduki wa London mwaka 2011 na kurudi kwenye klabu iliyomlea tangu akiwa mtoto ya Barcelona.
Alianza kucheza Ligi Kuu ya Uingereza mwaka 2003, lakini aliondoka Emirates kama ilivyo kwa nyota wengine, Thierry Henry, Patrick Vieira, Ashley Cole, Samir Nasri, Emmanuel Adebayor, Mathieu Flamini, Kolo Toure na Gael Clichy na kujiunga timu tofauti.
Mwezi uliopita pia, ripoti zilipindisha maneno ya Fabregas na kudaiwa
alisema hatakaa arejee Arsenal, na sasa Mhispania huyo mwenye umri wa
miaka 25 amesema yeye ni Arsenal damu.
“Sijazungumza na Wenger kuhusu hili, lakini ni habari njema kwangu, kwa sababu nilisikitika nilipoondoka.
“Nilipozungumza naye baadaye nilifurajia sana, kwa sababu niliweza
kushikana mkono naye na kumwangalia machoni. Nisingejilaumu daima kama
ningeondoka vibaya Arsenal, ni klabu kubwa, imenipa kila kitu.
“Nafarijika sana nikikumbuka mema mengi ya pale. Arsenal ndiyo chaguo
langu siku zijazo kama nitaondoka Barcelona. Ndiyo timu ya kwanza ya
chaguo langu, lakini kwa sasa hapa (Barcelona) sina tatizo,” anasema.
Barcelona walipokea kichapo cha mabao 2-0 kutoka kwa AC Milan kwenye
michuano ya Kombe la Mabingwa Ulaya, na Fabregas alizungumza na
waandishi kueleza kwamba watajitahidi kulipiza kisasi mechi ya
marudiano.
Fabregas alianza kuchezea timu ya chipukizi Barcelona 1997 kabla ya
kujiunga Arsenal 2003. Pia amechezea timu ya taifa ya Hispania ya vijana
chini ya miaka 16 na ile ya wakubwa.
No comments:
Post a Comment