CHAMA cha Waandishi wa
Habari za Michezo Tanzania (TASWA) kimefuta wazo la kuendesha mdahalo
kwa wagombea wa nafasi za juu za uongozi wa Shirikisho la Soka Tanzania
(TFF).
Mdahalo huo ulikuwa ufanyike Februari 15, 2013 na tayari chama
kilikuwa katika hatua nzuri ya mazungumzo na wadhamini pamoja na kituo
kimoja cha televisheni kwa ajili ya kurusha 'live' tukio hilo, ambapo
kesho ilikuwa tutangaze utaratibu mzima wa mdahalo huo. Katika
mazungumzo ya leo na uongozi wa kituo hicho ambao hautaki tukitangaze,
tumekubaliana kufuta wazo la mdahalo kwa sababu nafasi ya urais amebaki
mgombea mmoja, hivyo mdahalo hautakuwa na tija. Dhamira ya awali ya
kufanya mdahalo ilikuwa kuwapa fursa wapiga kura wasikie vyema sera za
wagombea urais na Makamu wa Rais, ili wananchi wawasikilize wagombea hao
na pia wapiga kura wawatambue vizuri.
Hata hivyo TASWA itatafuta
utaratibu mwingine mzuri ambao utawezesha wagombea kuzungumza na
waandishi wa habari na kuulizwa maswali mbalimbali ambayo tunaamini kwa
kiasi fulani yatasaidia wapiga kura katika uchaguzi unaotarajiwa
kufanyika Februari 24 mwaka huu. TASWA inawatakia kila la kheri wagombea
wote wa TFF waliobakia.
TASWA imekuwa ikifanya mdahalo kwa wagombea wa
nafasi za juu kwenye uchaguzi wa TFF, ilifanya hivyo mwaka 2001 na mwaka
2004 ingawa haukuwa wa live, ikafanya wa live mwaka 2008, ambapo yote
ilikuwa ya mafanikio makubwa.
No comments:
Post a Comment