Hali ya kifedha ndani ya klabu ya Simba imeanza kuibua hofu baada ya
kudaiwa kuwa kocha wao Mfaransa Patrick Liewig hajalipwa mishahara yake
ya miezi miwili huku pia akinyang'anywa gari alilokuwa akitumia kutokana
na uongozi wa klabu hiyo kutolipa madeni ya huduma walizopata katika
hoteli mbili jijini Dar es Salaam.
Taarifa kutoka ndani ya klabu hiyo zilidai jana kuwa kocha Liewig
amenyang'anywa gari alilokuwa akitumia aina ya Toyota GX110. ambalo
limeshikiliwa na hoteli moja ya Kariakoo jijini Dar es Salaam inayodai
Sh. milioni 28.
Imedaiwa kuwa baada ya kulimbikiza deni katika hoteli hiyo ya
awali, uongozi wa Simba ukahamia katika hoteli nyingine iliyopo pia
katika eneo la Kariakoo na kulimbikiza deni jingine linalozidi Sh.
milioni 20 na mwishowe, wakafukuzwa juzi baada ya uongozi wa hoteli
kuhofia kuwa watapata usumbufu katika kulipwa fedha zao.
Imeelezwa zaidi kuwa mbali na kushikiliwa kwa gari alilokuwa
akitumia Liewig, pia basi dogo la klabu hiyo linashikiliwa kwa sababu
ya madeni.
Uongozi wa Simba ulikiri kuzuiwa kwa timu yao kabla ya mechi ya
Ligi Kuu ya Tanzania Bara dhidi ya Coastal Union juzi kutokana na
kudaiwa na uongozi wa hoteli, lakini umekanusha kuwapo kwa taarifa
nyingine kuwa kuna hujuma kutoka kwa baadhi ya wanachama wa klabu hiyo.
Katibu Mkuu wa Simba, Evodius Mtawala,
amesema kwamba klabu hiyo inadaiwa jumla ya Sh. milioni 51 na hoteli
mbili za Kariakoo jijini Dar es Salaam; moja ikidai Sh. milioni 25 na
nyingine Sh. milioni 26.
Alisema madeni hayo yametokana na huduma walizokuwa wakipata kwa muda mrefu za malazi na chakula kwa wachezaji na makocha wao.
Mtawala amesema kwamba walishangazwa na tukio la kuzuiwa kwa timu
yao wakati hadi kufikia saa 6:00 mchana walikuwa na mmiliki wa hoteli
husika ambaye hakuonyesha kuwapo na nia hiyo aliyodai kuwa
imeidhalilisha timu yao.
"Sisi tunafanya nao biashara tangu msimu huu wa ligi ulipoanza
ambapo timu ikiwa na mechi Dar es Salaam na kila mechi inapochezwa siku
inayofuata tunamlipa kati ya Sh. milioni 8 na Sh.milioni 15... ila kwa
hili ametudhalilisha kwa sababu alipaswa atupe notisi," alisema Mtawala.
Katibu huyo aliongeza kuwa yote hayo yanatokana na timu yao kufanya
vibaya na hivyo kupata mapato kidogo ya milangoni, akitolea mfano mechi
dhidi ya Coastal waliyoambulia Sh. milioni 8 tu ambazo hazitoshi
kulipia madeni yanayowakabili.
"Tuko kwenye mazungumzo na wadau wetu pamoja na mama
Rahma...tunaweza kuwalipa jioni hii (jana jioni) au kesho (leo)
asubuhi," alisema Mtawala.
Aliongeza kuwa hata hivyo, Simba pia inazidai taasisi kadhaa na hivyo wanawaomba wanaowadai kuwa na subira kwani watawalipa tu.
Mtawala aliongeza kwamba kufuatia hali hiyo uongozi uko katika
hatua ya mwisho ya kuwalipia pango ya nyumba makocha wake pamoja na
wachezaji wa kigeni.
Mmiliki wa hoteli mojawapo inayoidai Simba, Abdul Fattah, alisema
kwamba hivi sasa hawataki klabu hiyo iendelee kulimbikiza deni kwa
sababu hakuna urafiki katika biashara.
Hivi karibuni, Simba imejikuta katika wakati mgumu kutokana na
matokeo yasiyoridhisha na kuwalazimu baadhi ya viongozi wake kujiuzulu,
wakiwamo makamu mwenyekiti wa klabu hiyo, Gofrey Nyange 'Kaburu' na
aliyekuwa mjumbe wa kamati ya utendaji na mwenyekiti wa kamati ya
usajili, Zacharia Hanspope.
No comments:
Post a Comment