KAMPUNI ya Bia
Tanzania (TBL) itadhamini bonanza la vyombo mbalimbali vya habari
litakalofanyika Aprili 6 mwaka huu viwanja vya Leaders Klabu, Dar es Salaam
likiandaliwa na Chama cha Waandishi wa Habari za Michezo Tanzania (TASWA).
Akizungumza katika
mkutano na wanahabari kutambulisha bonanza hilo Dar es Salaam jana, Ofisa
Uhusiano wa TBL, Doris Malulu alisema huu ni mwaka wa tano mfululizo kwa
kampuni yake kudhamini bonanza linaloandaliwa na TASWA na kwamba wamekuwa na
matumaini makubwa na chama hicho ndiyo sababu wanakubali kushirikiana nacho
kila mwaka.
Malulu alisema
zaidi ya Sh. Milioni 50 zitatumika kwa ajili ya bonanza hilo na kusisitiza kuwa
lengo la kampuni yake ni kuona linakuwa na mafanikio makubwa kuliko mengine
yaliyopita.
“Wanahabari ni
wadau wetu wakubwa, hivyo kupitia TASWA tunaona ni njia nzuri ya kutuunganisha
na kukaa pamoja kutafakari masuala mbalimbali,” alisema Malulu.
Kwa upande wake
Katibu Mkuu wa TASWA, Amir Mhando aliishukuru TBL kwa udhamini huo na kusema
kuwa zaidi wa washiriki 1,500 wanatarajiwa kuhudhuria tamasha hilo
linaloandaliwa na TASWA kila mwaka likijulikana kama Media Day Bonanza.
“Lengo la bonanza
letu ni kuwaweka pamoja waandishi wote wa habari bila kujali ni wa siasa,
michezo, uchumi, afya na mambo mengine pamoja na wafanyakazi wa vyombo
mbalimbali vya habari, ili kubadilishana mawazo na kufurahi pamoja,” alisema.
Alieleza kuwa bonanza
hilo litaambatana na michezo mbalimbali itakayohusisha vyombo vyote
vitakavyoshiriki na pia kutakuwa na burudani ya muziki kutoka katika moja ya
bendi kubwa za muziki wa dansi hapa nchini, ambayo itatangazwa siku zijazo.
Bonanza la mwaka
jana lilifanyika ukumbi wa Msasani Beach Klabu, ambapo mgeni rasmi alikuwa Waziri
wa Ushirikiano wa Afrika Mashariki, ambaye pia ni Mbunge wa Urambo Mashariki na
aliyekuwa Spika wa Bunge la Tisa, Samuel Sitta.
Pamoja na mambo
mengine, Sitta alikabidhi zawadi za vikombe na medali kwa washindi mbalimbali
walioibuka siku hiyo, pia alipata fursa ya kuzungumza na washiriki zaidi ya
1,500 wa bonanza hilo
No comments:
Post a Comment