kiungo mwenye kipaji kikubwa cha soka nchini Abdulhalim
Humud wa Azam amefuzu majaribio kwenye klabu kubwa ya soka ya Jomo
Cosmos ya Afrika Kusini Hii ni habari ya kusisimua, ya kufurahisha lakini si
ya kushangaza.
Inasisimua kwamba Humud anaingia kwenye orodha ya majina makubwa
katika soka ya Afrika ya kina Tico-Tico wa Msumbiji, Mark Fish, Phil
Masinga, Aaron Mokoena, Mark Williams wa Afrika Kusini, Bruce Globbelaar
wa Zimbabwe, Chris na Felix Katongo wa Zambia na wengine wengi wa
hadhi zao katika orodha ya wachezaji watakaowahi kuichezea timu hiyo ya
Afrika Kusini inayopigana kurudi kwenye ligi kuu (Premier Soccer League)
ya nchi hiyo baada ya kushuka daraja toka daraja hilo hadi la kwanza kwenye msimu wa 2009-10.
Hii ni habari ya kufurahisha kutokana na ukweli kwamba Humud
ameshinda majaribio ya kuchezea timu inayoweka mikakati mizito kurudi
ligi kuu. Ni wazi kufanikisha mikakati hiyo lazima timu hiyo inatafuta
vifaa vya uhakika na si vya ubabaishaji ili kufikia lengo lake. Kwa
msingi huo, ni wazi Humud ni kifaa kweli kweli.
Ukweli ni kwamba klabu yoyote yenye shinikizo fulani kubwa kama
juhudi za kupanda daraja, kuchukua ubingwa iliyoupoteza, kutetea ubingwa
iliyo nao, kutohangaika kutoshuka daraja kama msimu uliotangulia na
mengineyo, hutafuta wachezaji wa nguvu ili kufanikisha lengo husika. Kwa
hiyo Mtanzania Humud ni kifaa cha ukweli.
Habari hii haishangazi kwani Humud anaujua mpira kweli kweli. Ni
matatizo kadhaa, hasa majeraha ya mara kwa mara, ndiyo yamemuondoa
kwenye timu ya taifa na kupunguza uchezeshwaji wake kwenye timu yake ya
Azam. Huyu ni mchezaji ambaye watangazaji wa kituo cha runinga za
michezo cha Supersport cha Afrika ya Kusini walimshangaa, mara kadhaa
waliposhughulika na uonyeshaji wa mechi zetu toka Tanzania, kwa nini
hachezi soka ya kulipwa Ulaya au kwingineko kwenye soka kubwa.
Aidha, wachezaji na makocha wa timu maarufu za taifa za bara hili
tulizocheza nazo,Humud akicheza,kama Cameroon, Ivory Coast na Misri
walimsifu sana wakisema mchezaji huyo, mzaliwa wa Zanzibar, kucheza ligi
ya Tanzania si sahihi kwa kipaji chake cha hali ya juu.
Anachopaswa kufanya Mtanzania mwenzetu Humud kwenye ajira yake mpya
ni kutopuuza mazoezi, kufanya mazoezi kwa bidii, kujituma, kwa
kuzingatia maelekezo na kushiriki mazoezi hayo kila alipohitajika
kufanya hivyo na kuacha visingizio. Akipata nafasi ya kupangwa, acheze
kwa juhudi na maarifa kwa kufuata maelekezo na kuingiza ubunifu wake wa
kuleta manufaa inapojitokeza hali isiyotarajiwa uwanjani. Awe na nidhamu
ya hali ya juu wakati wote, heshima na upendo kwa wote na ajiepushe na
homa ya nyumbani (home sickness).
Malengo yake yawe kujitahidi ili afike mbali zaidi ya Jomo Cosmos
katika soka kwani bado ana miaka yakutosha ya kuucheza mchezo huo
ikizingatiwa kuwa amezaliwa tarehe 12/03/1987 na hivyo kuwa na umri wa
miaka 26 tu. Achagizwe kwa hilo na historia ya baadhi ya waliomtangulia
kuchezea timu hiyo. Kipa Globbelaar alichezea Liverpool ya Uingereza.
Mark Fish alifika Lazio ya Italy kisha Bolton Wanderers, Charlton
Athletic na Ipswich Town za Uingereza.
Aaron Mokoena, aliyechezea pia timu ya vijana ya Bayer Leverkusen ya
Ujerumani kisha timu za wakubwa za Ajax ya Uholanzi, Blackburn Rovers
na Portsmouth za Uingereza, alianzia kwenye timu ya vijana ya Jomo
Cosmos. Mark Williams alichezea Wolverhampton Wanderers ya Uingereza.
Hii ni mifano michache tu ambapo kama Humud atazingatia kuwa na
nidhamu na masuala ya kutopuuza mazoezi, kufanya mazoezi kwa bidii,
kujituma, kwa kuzingatia maelekezo na kucheza kwa juhudi na maarifa,
naye atafika huko kwani mpira anaujua na sasa atakuwa ndani ya klabu
inayoendeshwa kitaalam kama taasisi. Hata Azam yake inajitahidi kuwa
hivyo lakini inaangushwa na Utanzania unaoizunguka.
Inaleta raha sana wachezaji wa kulipwa wanavyoongezeka kama hivi.
Tuna Mbwana Samatta na Thomas Ulimwengu walio wafumania nyavu matata
sana. Sasa tunampata kiungo wa nguvu Abdulhalim Humud. Kwa changamoto
hii ya Humud, ni wazi timu yetu ya Taifa itajaza wachezaji wa kulipwa wa
nafasi zote hivi karibuni.
Abdulhalim Humud timiza wajibu wako vizuri Afrika ya Kusini lakini
ukijiwekea msimamo kuwa hapo uko njiani tu kuelekea Ulaya. Uwezo unao,
sababu ipo kwa hiyo jenga nia. Uwezo unao kwa sababu soka unaijua kwa
hiyo safari ya Ulaya inategemea uamuzi wako wa kujituma na kuwa na
nidhamu huko ugenini. Kila la heri Mtanzania mwenzetu Abdulhalim Humud
Mohammed.
www.tanzaniasport.com
No comments:
Post a Comment