Klabu ya Simba ya jijini Dar es Salaam imesema kuwa inaandaa barua ya
kuidai fidia ya Sh. bilioni 1.5 timu ya Azam kutokana na kitendo cha
klabu hiyo kuwashitaki wachezaji wake wanne kwa madai kwamba walipokea
rushwa ya Sh. milioni 7 ili wacheze chini ya kiwango katika mchezo
uliozikutanisha klabu hizo ambapo Azam ilifungwa magoli 3-1.
Hatua hiyo ya Simba inafuatia taarifa iliyotolewa na TAKUKURU juzi
ikieleza kwamba wachezaji wanne ambao ni Aggrey Morris, Deogratius
Munishi 'Dida', Erasto Nyoni na Said Morad hawana hatia.
Mwenyekiti wa Simba, Ismail Aden Rage,
alisema kuwa tayari klabu yake imeshawasiliana na mwanasheria wake
baada ya kupata nakala ya hukumu iliyotolewa na TAKUKURU na wakati
wowote kuanzia leo madai yao watayafungua kisheria.
Rage alisema kuwa wamefikia maamuzi hayo kutokana na klabu ya Simba
kudhalilishwa katika jambo hilo katika kipindi chote tangu uongozi wa
Azam ulipotangaza kwamba umewasimamisha wachezaji wake kwa kuwatuhumu
wamepokea fedha jambo ambalo halikuwa kweli.
"Ni jambo la kuidhalilisha Simba na kutudhalilisha wana-Simba wote, hatuwezi kuliacha hivi hivi," alisema Rage.
WACHEZAJI WALIOSIMAMISHWA
Wakizungumza kwa nyakati tofauti, nyota hao walisema kwamba
wanasikia faraja kubainika hawana hatia na kwa sasa hawawezi kusema nini
watafanya kwa sababu ni mapema mno.
"Mimi niko njiani natoka Zanzibar narejea Dar es Salaam,
tutakapokutana wote pamoja ndiyo tutaamua hatua ya kuchukua, kwa leo ni
mapema mno kusema chochote," alisema beki, Aggrey Morris jana mchana.
Jana jioni mmoja wa wachezaji hao aliliambia gazeti hili kwamba
amepigiwa simu na kocha wa timu hiyo, Stewart Hall, ambaye amewataka leo
asubuhi waonane na wahudhurie mazoezi.
KAULI YA AZAM
UONGOZI wa Azam ambao ulikuwa na kikao jana uliamua kuwarejesha katika timu wachezaji hao wanne ambao iliwasimamisha.
Katibu Mkuu wa Azam, Nassor Idrissa, alisema jana katika taarifa
yao waliyoiweka kwenye tovuti ya klabu kwamba wanawakaribisha wachezaji
hao kujiunga na timu kutokana na kutokutwa na hatia yoyote.
"Wachezaji hao wanakaribishwa rasmi kurudi kikosini Azam kwa ajili
ya kujiunga na mazoezi na wachezaji wenzao," ilisema kwa kifupi sehemu
ya taarifa ya klabu iliyotolewa jana saa 9 mchana.
Azam iliwasilisha barua ya malalamiko kwa TAKUKURU tangu Novemba 9
mwaka jana ikiwatuhumu nyota hao wanne kupokea rushwa kutoka Simba ili
wacheze chini ya kiwango.
Mechi hiyo wanayotuhumiwa ilikuwa ya mzunguko wa kwanza wa ligi
inayoelekea ukingoni sasa ambayo ilichezwa Oktoba 27 mwaka jana huku
Azam ikiwa na machungu ya kuchapwa magoli 3-2 dhidi ya Simba kwenye
mechi ya Ngao ya Jamii iliyofanyika Septemba 11 mwaka jana.
Licha ya kuwasimamisha nyota hao, Azam ilikuwa ikiendelea kuwapa mishahara wachezaji hao kama kawaida.
No comments:
Post a Comment