Mwendeshaji baiskeli Lance Armstrong ameelezea
kushangaa kwa kukabidhiwa adhabu ya maisha ya kutoshiriki katika
michezo, ilhali wanamichezo wenzake wamekuwa wakipigwa marufuku ya miezi
sita tu.
Katika sehemu ya pili ya mazungumzo yake na
Oprah Winfrey, mwanamichezo huyo mwenye umri wa miaka 41 alisema:
"Ninastahili kuadhibiwa. Lakini sidhani ninastahili hukumu ya kifo.
"Ningelitamani sana kupata nafasi ya kushindana, lakini hiyo sio sababu ya yale ninayoyafanya."
Kwa usiku wa pili, mazungumzo yake na Winfrey,
mwenye umri wa miak 58, yalipeperushwa katika muda ambao watazamaji
wengi walipata fursa ya kutizama televisheni, na yalionekana kote
duniani kupitia tovuti yake.
Mazungumzo hayo yalikuwa hewani kipitia kituo cha Winfrey cha televisheni nchini Marekani, OWN, yaani Oprah Winfrey Network.
Katika sehemu ya kwanza ya mazungumzo yao,
Mmarekani Armstrong hatimaye alikiri kutumia dawa za kuongezea nguvu
michezoni zilizopigwa marufuku, baada ya kukanusha kwa muda wa miaka
mingi, na huku akiibuka bingwa mara saba wa mashindano ya baiskeli ya
Tour de France.
Katika sehemu ya pili ya mazungumzo, Armstrong
alijizuia kulia, huku akielezea namna familia yake imeathirika kutokana
na vitendo vyake.
Kuhusu kutamani kurudi katika mashindano ya Tour
de France, Armstrong alielezea hana matumaini ya hayo kufanyika, lakini
akaongezea: “Ikiwa unaninuliza kama ningelipenda kushindana tena, jibu
ni, ndio, mimi ni mshindani kweli. Hayo nimeyafanya katika maisha yangu
yote. Ningelipenda kushindana na wengine.
“Kuna mambo mengi ambayo siwezi kuyafanya
kutokana na kupigwa marufuku. Lakini kama kuna nafasi, ningelipenda
kushiriki katika mbio ya marathon ya Chicago, nikiwa na umri wa miaka 50. Ndio.”
“Unapoitaja adhabu niliyokabidhiwa….nimepata
hukumu ya kifo, ikimaanisha siwezi kushindana. Sisemi nimeonewa, lakini
ni adhabu tofauti.”
Armstrong alisema kwa “ubinafsi” angelipenda
marufuku hiyo ya maisha iondolewe. “Lakini kwa hakika, sidhani hilo
litafanyika, na itanibidi kuishi kwa kuikubali hukumu hiyo.”
Tarehe 17 Oktoba, mwaka jana, mara tu baada
ya habari kuchapishwa kwama alikuwa ni mtu laghai, siku sita baadaye
wadhamini wake wa michezo walisitisha udhaimini wao, ikiwa ni pamoja na
makampuni makubwa kama Nike, watengezaji baiskeli Trek, na kampuni ya
kutengeneza pombe ya Budweiser, Anheuser-Busch.
Wakati huo ilidhaniwa Armstrong alipata
hasara ya dola milioni 30, lakini akizungumza na Winfrey, alisema
ilikuwa ni hasara ya dola milioni 75 kwa siku.
Zaidi ya watu milioni 4.3 nchini Marekani walitizama sehemu ya kwanza ya mazungumzo hayo katika televisheni ya Winfrey, OWN.
Wengine 600,000 nchini humo walitizama moja kwa moja kupitia tovuti yake ya Oprah.com.
No comments:
Post a Comment