Kikosi
cha mabingwa wapya wa Ligi Kuu ya Vodacom msimu wa 2012/2013 timu ya
Young Africans Sports Club leo asubuhi kimeanza mazoezi katika uwanja wa
Gombani mjini Pemba kujiandaa na mchezo wake wa mwisho dhidi ya timu ya
Simba SC, mchezo utakaofayika mei 18 katika dimba la uwanja wa Taifa
jijini Dar es salaam.
Yanga ambayo tayari ilishatwaa Ubingwa wa VPL kabla hata ya Ligi
kumalizika imewasili salama kisiwani Pemba ambapo leo asubuhi kocha mkuu
Ernie Brandts ameongoza mazoezi ya kikosi hicho kinachojiwinda kupata
pointi 3 dhidi ya Simba Sc.
Ikiwa imebakia takribani wiki moja
kabla ya mchezo wenyewe kufanyika, uongozi wa klabu ya Yanga kwa
kushirikiana na benchi la ufundi uliamua kubadilisha mazingira ya kambi
kutoka makao makuu ya klabu mpaka kisiwani Pemba kuhakikisha wachezaji
wanapata mafunzo katika hali iliyo tulivu zaidi.
Akiongea mara
baada ya kumalizika kwa mazoezi hayo, kocha Brandts amesema
amefurahishwa kwa mapokezi ya wakazi wa kisiwa cha Pemba, kwani licha ya
kuja kuweka kambi ya kujianda na pia wamepata fursa ya kubadilisha
mazingira na kujifua vizuri katika hali iliyo tulivu.
Kuhusiana na
hali ya kikosi Brandts alisema kikosi chake kipo fit kiaklil, kifikra
na morali ya hali ya juu kuelekea kwenye mchezo hali inayoendelea kumpa
uhakika zaidi wa kuondoka na pointi 3 katika mchezo huo wa mei 18.
Aidha
Brandts akliongeza kuwa wachezaji wangu wote wapo salama, hakuna
mgonjwa wala mchezaji majeruhi hivyo kuja kuweka kambi kisiwani Pemba
kumeniongezea fursa ya kukaa na wachezaji wangu wote kwa pamoja, kuwapa
mbinu mbalimbali kwa pamoja na kupanga jinsi ya kuibuka na ushindi dhidi
ya Simba SC.
Uogozi wa klabu ya Yanga unawaomba wapenzi,
wanachama na washabiki wake wote kwa pamoja kujitokeza kwa wingi katika
mchezo wa mei 18 dhidi ya Simba Sc kwani licha ya kucheza na watani wa
jadi pia itakua ni siku ambayo Yanga itakabidhiwa rasmi kombe la Ubingwa
wa VPL 2012/2013.
No comments:
Post a Comment