BOFYA HAPA
Shirikisho la Mpira wa Miguu Tanzania (TFF) limeamua kurejesha ofisi
zake Uwanja wa Kumbukumbu ya Karume kwa vile mipango ya uendelezaji wa eneo
hilo bado haijakwenda kama ilivyopangwa awali.
Uendelezaji wa eneo utafanyika wakati ofisi zikiwa hapo hapo, na
Shirikisho la Kimataifa la Mpira wa Miguu (FIFA) litasaidia katika uendelezaji
huo utakaofanyika kwa awamu.
Vilevile FIFA imeahidi kusaidia uboreshaji wa ofisi za Uwanja wa Karume
ili ziwe katika mazingira bora zaidi ya kufanyika kazi.
Uamuzi huo ni moja ya maazimio yaliyofikiwa kati ya Kamati ya Utendaji
ya TFF na ujumbe wa Shirikisho la Kimataifa la Mpira wa Miguu (FIFA) uliokuwepo
nchini kwa wiki nzima kwa ajili ya kufanya mapitio (review) ya uendeshaji wa
TFF.
Akizungumza Dar es Salaam leo (Agosti 17 mwaka huu), kiongozi wa ujumbe
huo wa FIFA uliokuwa na maofisa sita, Zelkifli Ngoufonja amesema wamepitia
maeneo mbalimbali ya uendeshaji wa TFF na mpira wa miguu kwa ujumla na
kukubaliana kufanya uboreshaji kwa lengo la kuongeza ufanisi.
Ngoufonja ambaye ni Meneja Mwandamizi wa FIFA anayeshughulikia Programu
za Maendeleo Afrika amesema kabla walikutana na wadau mbalimbali ikiwemo
Serikali kwa lengo la kuangalia jinsi watakavyochangia katika uendelezaji mpira
wa miguu nchini.
Amesema wamekubaliana na TFF katika mpango wa utekelezaji (Action Plan)
na maazimio waliyokubaliana ikiwemo na muda wa utekelezaji wake, hivyo FIFA
watafuatilia na kutoa msaada ili kuhakikisha utekelezaji unafanyika kama
ilivyopangwa.
Maeneo yaliyofanyiwa kazi ni utawala bora (Governance), Maendeleo ya
Ufundi (Technical Development), timu za Taifa (National teams), Mashindano na
Vitendea Kazi (Competitions and Facilities), na Utawala na Uongozi
(Administration and Management).
Maofisa wengine wa FIFA waliofuatana na Ngoufonja ambaye ni raia wa Cameroon
ni Meneja wa Programu za Ustawi (Performance), Marco Schuepp, Ofisa Maendeleo,
Ashford Mamelodi, Ofisa Maendeleo wa Ufundi, Govinden Thondoo, Mkufunzi wa
Makocha, John Peacock na Mshauri wa Programu za Ustawi, Ian Riley.
MUDA WA USAJILI WAONGEZWA KWA SIKU KUMI
Shirikisho la Mpira wa Miguu Tanzania (TFF) limeongeza
kwa siku kumi muda wa kumalizika usajili wa wachezaji wa klabu za Ligi Kuu ya
Vodacom (VPL) na Ligi Daraja la Kwanza (FDL) kutokana na kuchelewa kwa link ya mfumo mpya
wa usajili (system) kutoka Shirikisho la Mpira wa Miguu Afrika (CAF).
Kwa mujibu wa CAF, link hiyo itakuwa tayari kwa
matumizi ndani ya siku tatu zijazo kutokana sasa. Hivyo, mameneja wa usajili wa
timu hizo kwa sasa wanatakiwa kukamilisha nyaraka zote zinazotakiwa ili link
hiyo itakapokuwa tayari waweze kuingiza usajili wao mara moja.
Kuanzia msimu wa 2014/2015 mfumo unaotumika kwa
usajili kwa klabu hizo ni wa elektroniki badala ya ule wa zamani wa kutumia
fomu za kawaida. Mfumo huo wa kisasa ambao pia unatumiwa na CAF unaondoa
upungufu uliokuwepo katika mfumo wa zamani.
Kutokana na mabadiliko hayo, usajili sasa utamalizika
Agosti 27 mwaka huu badala ya leo (Agosti 17 mwaka huu). Kipindi cha pingamizi
ni kuanzia Agosti 28 mwaka huu hadi Septemba 3 mwaka huu.
Kamati ya Sheria na Hadhi za Wachezaji itakutana kati
ya Septemba 6 na 8 mwaka huu kwa ajili ya kupitia pingamizi na kuthibitisha
usajili.
Ligi Kuu ya Vodacom (VPL) inayoshirikisha timu 14
itaanza Septemba 20 mwaka huu wakati ratiba inatarajia kutoka mwezi mmoja kabla
ya kuanza ligi hiyo. Ligi Daraja la Kwanza inatarajia kuanza wiki ya kwanza ya
Oktoba.
Mwisho wa kuombewa Hati ya Uhamisho ya Kimataifa (ITC)
kwa wachezaji wanatoka nje ya Tanzania ni Septemba 6 mwaka huu.
No comments:
Post a Comment